BILA mafanikio makubwa kwa muda mrefu, serikali imekuwa ikibuni mikakati ya kuangazia matatizo ya wizi wa mifugo, kiangazi na ukosefu wa maji katika Kaunti ya Baringo na maeneo mengine kame nchini.
Waziri wa Maji Eric Mugaa anaamini jamii zinazoishi Baringo zinaweza kukumbatia kilimo kikamilifu badala ya kutegemea sana ufugaji.
Kulingana na Mugaa, haya yote yatawezeshwa iwapo serikali itakita programu nzuri za kuhakikisha kuna utoshelevu wa maji ili kuangazia masaibu ya wakazi.
“Sasa ni wakati wa Baringo kunufaika na miradi ya maji. Kaunti hii inafaa kujitosheleza na kuwa na chakula kupitia kilimo cha unyunyiziaji. Hii itaondoa mzozo wa malisho na maji baina ya wafugaji,” akasema Bw Mugaa akiwa katika ziara ya siku mbili eneo hilo.
Kufikia sasa, wakazi wa eneobunge la Tiaty wamezidisha desturi ya kilimo cha umwagiliaji zaidi ya utamaduni wao wa jadi wa ufugaji.
Safari ya ufikiaji wa utoshelevu wa chakula umeanza kuwezeshwa na skimu ya unyunyiziaji maji ya Komolion, mradi wa majaribio katika shamba la hekta 100.
“Kitambo, tulikuwa tunatumia mafuta mengi kuendesha jenereta ili kuvuta maji hadi shambani. Lakini sasa inakuwa rahisi kwetu kukumbatia kilimo na kufurahia faida,” akasema mkulima wa Tiaty Joseph Chepkong’a.
Vile vile, serikali imeanzisha mradi wa unyunyiziaji wa Cheraik kuendeleza shughuli za zaraa eneo la Eldama Ravine.
Hii inalenga kunufaisha wakulima zaidi ya elfu moja pamoja na mpango sawa na huo katika eneobunge la Mogotio.
Mbunge wa Eldama Ravine Bw Musa Sirma amewahimiza wakazi kukumbatia upatikanaji huu wa maji kujiendeleza kiuchumi.
“Ni wakati mzuri kwenu kujikuzia chakula chenu kama vile kilimo cha nyanya ili kujitafutia mali,” akasema Bw Sirma.
Kulingana na Waziri Mugaa, uchimbaji wa mabwawa ya maji kama ule wa Radat, utaweka thabiti upatikanaji wa maji na kuangazia uhaba unaoshuhudiwa katika skimu ya Perkerra.
“Tunajaribu kuchunguza uwezekano wa serikali kutumia maji ya ziwa Baringo kufanikisha kilimo katika maeneo kame ya kaunti hii,” alisema waziri.
“Iwapo mabwawa mengi yatachimbwa na kuzidisha kiwango cha maji eneo hili, maisha ya wakazi yataimarika,” aliungama Bw Charles Kamuren, Mbunge wa Baringo Kusini.
Mradi wa unyunyizaji maji wa Perkerra ndio mkongwe zaidi baada ya kuundwa 1956.
Uchakavu wake bila kushughulikiwa ipasavyo, umesababisha uhaba wa maji na migogoro ya kupigania bidhaa hii adhimu.
Imetafsiriwa na Labaan Shabaan
Leave a Reply