Mkaguzi wa hesabu aanika basari kwa wanafunzi hewa katika maeneo bunge – Taifa Leo


RIPOTI ya ukaguzi imeonyesha kwamba, huenda mamilioni ya pesa za basari zilizokusudiwa kufaidi wanafunzi kutoka familia masikini, zinaishia katika mifuko ya maafisa na wabunge wafisadi katika maeneo bunge mbalimbali nchini.

Ripoti hiyo ya kusikitisha inajiri wakati wanafunzi wanaripoti shuleni kwa muhula wa kwanza 2025.

Ripoti ya hivi punde zaidi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu, iliyotolewa Desemba 2024, imefichua ubadhirifu wa fedha za Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneobunge (NGCDF), na hivyo basi kuwaacha wanafunzi kutoka familia maskini wakihangaika.

Ripoti hiyo inaonyesha jinsi fedha zilizokusudiwa kuwakinga wanafunzi hao zinavyoibwa katika maeneobunge mbalimbali, na basari kutolewa kwa wanafunzi hewa.

Aidha, hakuna maelezo ya majina ya taasisi za elimu, maelezo ya benki, kiasi cha basari, majina kamili ya wanafunzi na namba zao za usajili au barua au risiti kutoka kwa taasisi zinazosajili wanafunzi zilizowasilishwa kwa ukaguzi, ili kuthibitisha kuwa basari hizo zilipokelewa na taasisi za elimu.

“Kwa hivyo, haikuweza kufahamika, kama fedha za basari za mamilioni ya shilingi, zilizotolewa katika mwaka huo ziliwafikia walengwa na kuhesabiwa ipasavyo,” inasema sehemu ya ripoti ya ukaguzi wa mwaka wa fedha uliomalizika 2022.

Maeneobunge yaliyoathiriwa ni pamoja na; Sabatia, Rongo, Nakuru Mashariki, Narok Magharibi na Embakasi Kaskazini.Mengine ni; Webuye East,Turbo ,Suba North,Sotik,Nyaribari Chache, Naivasha, Mwingi Central, Mogotio, Olkalou, Nyakach,Malindi na Westlands miongoni mwa mengine.

Hakuna maelezo

Kulingana na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, katika eneo bunge la Sabatia, Kaunti ya Vihiga, Sh58 milioni zilitumika kwa basari, lakini ni Sh38 milioni pekee zilizoangaziwa bila maelezo ya walionufaika na kiasi cha fedha ambacho kila mwanafunzi alipokea. Huko Rongo, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alimulika taarifa ya malipo ya kima cha Sh65,643,718 za basari.

Hata hivyo, mapitio ya stakabadhi za malipo, ratiba na rekodi zilizotolewa kwa ukaguzi zilionyesha ratiba ya malipo ya basari ya jumla ya Sh2,118,500 hazikuakisi nambari za usajili za wanafunzi waliodaiwa kunufaika.

Kulingana na ripoti hiyo, wanafunzi 157 walipata mgao wa basari wa zaidi ya mara moja na wa viwango tofauti.

“Katika hali hiyo, matumizi ya kawaida ya Sh46,658,356, haki na usawa katika ulipaji wa basari katika eneobunge la Rongo haukuweza kuthibitishwa,” alisema Gathungu.

Katika Eneobunge la Narok Magharibi linalowakilishwa na Gabriel Tongoyo, Gathungu alimulika matumizi ya pesa zilizokusudiwa kufadhili masomo.Kwa mfano, basari za thamani ya Sh 9 milioni zilitumika visivyo kwa wanafunzi 675 bila nambari za usajili za shule.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa baadhi ya walionufaika katika Narok Magharibi walikuwa na nambari sawa za wanafunzi walioandikishwa katika shule zao na baadhi ya wanafunzi hawakuwa na majina.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Sh17,564,000 zilitolewa kama basari kwa shule za sekondari na Sh35,459,194 kwa vyuo vya elimu ya juu.

“Katika hali hiyo, uhalali, usahihi na ukamilifu wa malipo ya basari ya Sh17,895,194 na Sh17,564,000 kwa shule za upili na vyuo vya elimu ya juu katika eneo bunge la Narok Magharibi hayakuweza kuthibitishwa,” alisema Gathungu.

Embakasi Kaskazini

Huko Embakasi Kaskazini, linalowakilishwa na James Gakuya, Gathungu alisema ‘uchunguzi wa stakabadhi za malipo zilizotolewa kwa ukaguzi zilibaini Sh58,820,000 za basari katika eneobunge la Embakasi Kaskazini zilisababisha tofauti isiyoeleweka ya Sh605,000.

Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alisema kati ya Sh46,465,000 zilizotolewa kwa shule za sekondari za eneo hilo, kuna malipo ya Sh34,000,000, ambayo ratiba ya shule na walionufaika haikutolewa kwa ukaguzi.

Katika Nyaribari Chache, ukaguzi ulibaini kuwa hakukuwa na kamati ya iliyoanzishwa ipasavyo licha ya Sh 92 milioni kulipwa katika mwaka ambao ukaguzi ulifanywa.

Maeneo mengine ambayo hayawezi kuthibitisha mamilioni ya shilingi zilizotolewa kwa shule za sekondari, vyuo vya elimu ya juu na shule maalum ni pamoja na; Sotik (Sh35 milioni), Naivasha (Sh64 milioni), Mwingi ya Kati (Sh77 milioni), Mogotio (Sh103 milioni), Olkalou (Sh48 milioni), Nyakach (Sh56 milioni.)

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*