Mke alivyoua mume kwa asidi kwenye mzozo wa kimapenzi – Taifa Leo


MWANAMKE mmoja kaunti ya Nakuru alikamatwa aliporipoti katika kituo cha polisi baada ya mumewe kufariki kwa kuchomwa na asidi.

Claris Mghoi binti ya mke mwenza wa mwanamke huyo, alieleza kwamba, kabla ya kufariki, babake alimwlelelezea jinsi mkewe alivyommwagia asidi mwilini.Alisema kabla ya kupata habari za masaibu ya babake, mnamo Alhamisi Desemba 5, 2024, hakufahamu kuwa maisha yake yalikuwa karibu kubadilika.

Ni mjomba wake aliyepiga simu akimtaka asafiri kwa haraka kutoka kazini kwake Kericho hadi Nakuru.

“Aliniambia baba yangu hakuwa akihisi vizuri na kwamba nilihitaji kuja mara moja. Hakuniambia kilichotokea na alitoa maelezo machache akaniacha nikiwa na hofu,” Bi Mghoi aliambia Taifa Leo.

blanketi lililoungua 

Alipofika Nakuru baadaye siku hiyo, alienda moja kwa moja kwa nyumba ya babake katika mtaa wa Kaptembwa ambako alikuwa akiishi na mke wake wa pili kwa miaka sita.Lakini tukio alilokumbana nalo lilikuwa la kusikitisha.Kulikuwa na fanicha zilizopinduliwa, vitu vikiwa vimetawanyika na blanketi lililoungua likiwa sebuleni.

“Nilichokiona pale nyumbani kiliniacha hoi, mambo yalikuwa yamevurugika tu. Nilijaribu kuwauliza majirani lakini hakuna aliyekuwa akiniambia jambo la kuridhisha. Katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nakuru, ndipo nilipokumbana na hali halisi, babangu alikuwa ameungua vibaya, alikuwa na maumivu makali,” alisimulia katika mahojiano na Taifa Leo mnamo Alhamisi.

Babake, Elijah Matoke Maina, 52, alikuwa amelala kwa maumivu makali, mwili wake ukiwa umejaa majeraha ya moto yaliyotokana na asidi. Siku tano baadaye, alifariki dunia na kuiacha familia yake ikiwa imevunjika moyo na kudai haki itendeke.Katika siku zake za mwisho, Bw Matoke alimweleza binti yake matukio ya kuhuzunisha ya usiku huo wa balaa.

Kulingana na Bi Mghoi, aliyerekodi mazungumzo hayo, babake alielezea jinsi mkewe alivyoamka mwendo wa saa tatu asubuhi na kuanza kupekua masanduku chini ya kitanda chao. “Alikuwa akitafuta kitu lakini alisema hakufuatilia sana,” alisema.

Bi Mghoi alidai katika taarifa yake kwa polisi kwamba inasemekana mke wa babake aliondoka nyumbani na kurudi na kontena la lita tano. Alidhani ni maji lakini ikawa ni asidi ambayo anadaiwa alimmwagia.

Mayowe

“Alisema maumivu hayakuweza kuvumilika,”Bi Mghoi alisema. Mayowe yake yaliwaamsha watoto wao wadogo ambao walikimbia kuona kilichotokea. Majirani nao walivutiwa na zogo hilo na kusaidia kumkimbiza Bw Matoke hospitalini.

Wakati huo huo, mkewe alitoroka na kutokea tena baadaye akiwa na majeraha ya moto mikononi mwake.Bi Mghoi alisema ndoa ya pili ya babake ilikuwa yenye matatizo kwa miaka mingi.

Baada ya kutengana na mamake 2012, Bw Matoke alioa tena na kuhamia Nakuru.Alisema kuwa wakati huo, baba huyo alimuomba asafiri kutoka Kericho, baada ya kumtambulisha kwa mwanamke huyo, alimweleza kuwa alitaka kuoa tena, uamuzi ambao hakuupinga.Licha ya mvutano huo, Bw Matoke alijaribu kudumisha ndoa hiyo.

“Alikuwa rafiki yangu mkubwa. Hakuwa mtu jeuri, alipendwa na watu na hakustahili hili. Tulikuwa na mipango mingi sana na baba yangu. Tunawaomba polisi kufanya uchunguzi wa haraka ili baba yangu apate haki ili apumzike kwa amani,” alisema.

Kaka ya Bw Matoke Bernard Angwenyi alisema uhusiano wa wanandoa hao ulijaa migogoro ambayo nyakati fulani iligeuka kuwa ya vurugu.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*