NI mwishoni mwa mwaka jana tu ambapo mke wa Kyle Walker, Annie Kilner, alikuwa akijiandaa kubwagana na sogora huyo baada ya kuomba talaka.
Demu huyo aliapa kupigana vita vikali vya kisheria katika juhudi za kutaka nusu ya utajiri wa Walker unaokadiriwa kufikia Sh4.5 bilioni.
Annie sasa amepiga abautani baada ya kuibuka kwa tetesi zinazomhusisha Walker, 34, na uwezekano wa kuhamia Saudi Arabia kwa kima cha Sh3.2 bilioni ili kuchezea Al-Nassr, Al-Ahli au Al-Ittihad kwa mshahara wa hadi Sh64 milioni kwa wiki.
Wale walio karibu na Annie, 33, waliambia gazeti la The Sun kwamba kipusa huyo ameweka breki kwa sasa mpango wa talaka huku akimrudisha Walker ambaye ni beki wa Manchester City na timu ya taifa ya Uingereza katika nyumba yao ya ndoa.
Walker, ambaye kwa sasa analipwa mshahara wa Sh25 milioni kwa wiki, alifukuzwa na Annie katika kasri lao la Sh630 lililoko eneo la Prestbury, Cheshire, mwishoni mwa 2023 baada ya Lauryn Goodman, 34, kufichua kwamba beki huyo alikuwa amepata naye mtoto wa pili. Annie wakati huo alikuwa akitarajia kujifungua mtoto wake wa nne pamoja na Walker.
Hata hivyo, Walker na Annie waliitisha mapatano wakati wa Krismasi ya 2024 kwa ajili ya watoto wao wanne – Roman, 12, Riaan, 8, Reign, 6, na Rezon aliyezaliwa Aprili 2024.
Sogora huyo alinaswa na kamera akishiriki mlo wa Krismasi pamoja na Annie na watoto wao kabla ya kuungana baadaye na wachezaji wenzake wa Man-City.
Iliripotiwa kwamba hakutuma zawadi yoyote ya Krismasi kwa Kairo na Kinara – watoto wake wawili na mwanamitindo Lauryn ambaye ni mpango wake wa kando.
“Ni miezi michache tu iliyopita ambapo Annie alimpokeza Walker stakabadhi za talaka. Sasa amebadilisha mawazo baada ya kubaini kwamba beki huyo atakuwa na ushawishi mkubwa wa kifedha akihamia Saudi Arabia. Amemrejesha Walker nyumbani na hafichi tena pete ya ndoa aliyoapa kuvua hapo awali,” akasema mdaku aliyehojiwa na The Sun.
Annie alianza kutoka kimapenzi na Walker akiwa na umri wa miaka 16 baada ya kukutana mjini Sheffield. Walifunga pingu za maisha mnamo Novemba 2021 katika ukumbi wa Mottram huko Cheshire, Uingereza.
Hata hivyo, ndoa yao ilianza kuyumba kutokana na jicho la nje la Walker aliyeanza kuchovya asali ya vipusa Carla Howe, Laura Brown na Lauryn.
Leave a Reply