MCHEZAJI wa zamani wa timu ya AFC Leopards na Western Stima Ezekiel Otuoma 31, amefariki dunia Desemba 21, 2024 baada ya kuugua uvimbe wa neva kwa kipindi cha miaka minne.
Mkewe Rachel Otuoma ambaye amekuwa akimuuguza, alichapisha taarifa kwenye ukurasa wake wa TikTok kwa kumpoteza mpenzi wake.
“Kwa mume wangu, umewacha moyo wangu ukiwa na shimo ambalo haliwezi kujazwa. Upweke mikononi mwangu unanikumbusha upendo tuliokuwa nao…ila imekuwa hivi. Umeacha moyo wangu ukiwa umevunjika kwa kuniacha siku yangu ya kuzaliwa, haitawahi kuwa sawa tena… Inauma kuniacha lakini hujaenda pekee yako ila kipande changu kipo na wewe,” ilisema taarifa hiyo.
Mchezaji huo aliugua ugonjwa wa uvimbe wa neva mwilini kuanzia mwaka wa 2020. Mwaka 2023, Bi Otuoma alisema kuwa mumewe alianza kupoteza uwezo wa kuzungumza wakati wa mawimbi ya Covid-19 na kisha mishipa yake ikakosa nguvu na kusababisha kukosa kutembea pamoja na kushika vitu kwa mikono yake.
Katika kipindi hicho cha miaka minne cha kumuuguza mumewe, Bi Otuoma alilalamikia kupitia dhuluma kutoka kwa familia yake pamoja na wana mitandao.
“Nashangaa kuona familia ikidai kuwa napata pesa kupitia mitandao ya kijamii kupitia kwa mwana wao. Cha kusikitisha ni kuwa mamake Otuoma hajawahi kuja kumuona mwanawe tangu aanze kuugua. Hawajawahi kusema wanamchukua waende naye. Nimebaki kumshughulikia pekee yangu,” alisema Machi 2024, kwenye mtandao wa TikTok.
Rachel alisema kwamba tangu 2020 ambapo ugonjwa huo ulipoanza kumuathiri mume wake, maisha yao yalibadilika.
“Imekuwa miaka minne ambayo imejaa changamoto sio haba, kumuona mwanamume ambaye alikuwa ananihudumia kwa yote akiwa hawezi chochote sio rahisi ila ninajikakamua kila siku nikitumai ya kwamba atapona,” aliongeza.
Timu za AFC Leopards, Western Stima na Talanta FC zimemwomboleza mshambuliaji huyo wa zamani aliyefariki usiku wa kuamkia Jumamosi hospitalini.
Timu ya Sofapaka pia ilimtaja kama shujaa aliyekamilisha safari yake duniani ila mchezaji ambaye hatosahaulika na atakayesalia katika kumbukumbu za wachezaji bora nchini Kenya.
Leave a Reply