
UJENZI wa mradi wa Nairobi Railway City, unaotarajiwa kuanza Aprili mwaka huu, unalenga kufungua nafasi za ajira kwa vijana zaidi ya 5,000.
Mradi huu mkubwa, unaofadhiliwa na serikali ya Uingereza una nafasi kubwa ya kubadilisha sio tu mandhari ya jiji la Nairobi bali pia kuinua uchumi wa taifa.
Mbali na ajira za moja kwa moja 5,000 zitakazoundwa wakati wa ujenzi, nafasi zingine za ajira 5,000 zitaundwa baada ya kukamilika kwa awamu ya pili na ya kwanza ya ujenzi.
Aidha, kutakuwa na nafasi nyingi za biashara kwa wafanya biashara ndogo ndogo.
Mradi huu unajumuisha maendeleo ya miji yanayozingatia usafiri wa kisasa kwa njia mbalimbali, lengo likiwa ni kuboresha jiji na kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia utekelezaji wa mpango wake mkuu.
Ujenzi wa mradi huo utachukua ekari 425 za ardhi ambayo kwa sasa haitumiki kikamilifu hasa katika kitovu cha jiji la Nairobi (CBD).
Sehemu kubwa ya ardhi hii inamilikiwa na Shirika la Reli la Kenya, Mpango wa Mafao ya Wafanyakazi wa Shirika la Reli la Kenya (KRSRBS), na mashirika mengine ya serikali.
Akisifia mradi huo, rais wa Bunge la Mwananchi Francis Awino alisema kuwa mradi huo utasaidia sana kushughulikia suala la msongamano wa magari CBD.
“Hii imekuwa tatizo kwa muda mrefu ila ujenzi wa mradi huo ambao kwetu sisi tunauchukulia kama mradi wa wananchi utasaidia pakubwa kushughulikia suala la msongamano wa magari,” akasema Bw Awino.
Kando na hayo, alisema kuwa vijana watapata ajira kupitia mradi huo, jambo ambalo litawainua kiuchumi.
“Tunajua kuwa vijana wengi hawana ajira, ila kupitia mradi huu, vipana 5,000 watapata ajira,” akaongeza.
Mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya Uingereza utagharimu mamilioni ya fedha.
Leave a Reply