MSANII nguli wa Uganda Jose Chameleone ametua Boston, Amerika, kwa matibabu maalumu baada ya kuondoka hospitali moja jijini Kampala alikolazwa kwa muda.
Ripoti zilisema msanii huyo aliwasili Amerika mapema wiki hii na kupokelewa na kakake mdogo na mwanamuziki mwenzake, Weasel, ambaye amekuwa akiratibu mipango ya matibabu yake ng’ambo.
Chameleone sasa anajiandaa kupata matibabu huko Boston, hatua ambayo familia yake na marafiki wanaamini itatoa huduma ya hali ya juu anayohitaji kushughulikia changamoto zake za kiafya zinazoendelea.
Mwanamuziki huyo alisikitika kuwa kwa mara ya kwanza katika miaka mingi hakuweza kutumbuiza mashabiki wake msimu wa sherehe za Krismasi na mwisho wa mwaka.
Kusafiri kwake Amerika kunafuatia kipindi cha kutokuwa na uhakika na mjadala kuhusu iwapo alifaa kusalia katika Hospitali ya Nakasero ya Kampala au kutafuta matibabu ng’ambo tovuti ya Chimpreports ilisema.
Uamuzi wa kumsafirisha Chameleone kwenda Amerika ulijiri huku mwanawe, Abba Marcus Mayanja, akifichua kwamba mwimbaji huyo amekuwa akipambana na matatizo yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya.
Ombi la Abba kwa mashabiki na watu wenye mapenzi mema lilionyesha dharura ya hali hiyo.
“Tunahitaji kuungana na kumsaidia kama tunataka kumweka katika familia yetu,” Abbas alisema, akitoa wito kwa mashabiki kumuunga mkono baba yake.
Kulingana Chimpreports, madaktari katika Hospitali ya Nakasero awali walikuwa wameonya dhidi ya kumhamisha Chameleone, wakitaja hali yake dhaifu na hatari zinazohusishwa na safari ndefu ya ndege.
Pia walisisitiza kuwa hospitali hiyo ina utaalamu na vifaa vinavyohitajika kushughulikia hali yake.
Hata hivyo, marafiki wa karibu wa Chameleone na familia, wakiongozwa na mwanamuziki Sarah Zawedde, walichagua kumsafirisha hadi Amerika, wakiamini kuwa matibabu maalum nje ya nchi yatamwezesha kupona.
Chameleone, anayejulikana kwa mchango wake mkubwa katika muziki wa Afrika Mashariki, bado ni mmoja wa wasanii maarufu zaidi katika ukanda huu.
Leave a Reply