
UMATI wa maafisa wa polisi wa Congo waliojiunga na waasi wa M23 waliimba na kupiga makofi mjini Bukavu Jumamosi, wakijiandaa kupokea mafunzo upya chini ya uongozi wa kundi hilo linalopania kudumu na kutawala eneo hilo.
Waasi wa M23 waliingia wiki iliyopita katika mji wa pili mkubwa zaidi Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo uliokumbwa na uporaji na ghasia huku vikosi vya jeshi la Congo vikiondoka bila kupigana.
Kitendo cha M23 kuteka maeneo makubwa Congo Mashariki na vituo vyenye madini ya thamani kimezidisha hofu ya mapigano makali kuzuka na kusababisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuagiza kwa pamoja waasi hao kusitisha uhasama na kujiondoa.
Hakukuwa na ishara wito huo ungezingatiwa Bukavu. Polisi waliokusanyika wakiwa wamevalia sare mpya na kofia nyeusi, walielezwa wataondoka kwa siku chache za mafunzo na kurejea kusaidia M23.
“Mrejee kwetu mkiwa wazima ili pamoja tuendelee kulikomboa taifa letu,” alisema Kamanda wa Polisi Jackson Kamba.
Maafisa wa polisi wapatao 1,800 wamejisalimisha na wamekwenda kupokea mafunzo upya huku 500 wakisubiri kufuata mkondo, alisema msemaji wa muungano wa waasi AFC unaojumuisha kundi la M23, Lawrence Kanyuka.
Serikali ya Congo haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni.
Michafuko inayoendelea Mashariki mwa DRC inazidi kushika kasi na taharuki baina ya serikali ya Rais Felix Tshisekedi na waasi wa M23.
Leave a Reply