AFISA mmoja wa polisi aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Kaunti-ndogo ya Bondo Jumatatu aliwadunga visu wagonjwa wawili kabla ya kuzuiliwa na wenzake.
Ni tukio lililowashangaza wengi japo inaaminika afisa huyo alikuwa na matatizo ya kiakili. Afisa huyo, Mohamed Gure aliwaacha wagonjwa hao wakiwa na majeraha mabaya.
Gure, ambaye anadumu katika kituo cha polisi cha Aram, Kaunti-ndogo ya Rarieda, alilazwa hospitalini humo alikokuwa akipokea matibabu kabla ya kudunga wagonjwa wengine visu.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti-ndogo ya Bondo Robert Aboki alisema kuwa polisi waliingilia kati na kumzuia Gure kuwajeruhi wagonjwa wengine zaidi.
“Kwa sasa hakuna hatari kwa sababu tumemdhibiti. Hata hivyo, tuko kwenye mchakato wa kusaka matibabu spesheli kwake na madaktari na maafisa wengine wanafanyia kazi hilo,” akasema Aboki.
Wagonjwa ambao walijeruhiwa wako katika hali thabiti wala hawako hatarini. “Wagonjwa wako hali imara na huduma katika hospitali hiyo zinaendelea bila tatizo lolote,” akaongeza.
Supritendi wa hospitali hiyo Evans Ogoti alisema polisi wanaendeleza uchunguzi huku usalama ukiimarishwa ili watu wapokee huduma bila tatizo lolote,” akasema Dkt Ogoti.
Dkt Ogoti alisema afisa huyo alikuwa amelazwa hospitalini humo akiendelea kupokea matibabu kama wagonjwa wengine.
Ingawa hivyo, hospitali bado haijatoa maelezo kamili kuhusu afya ya afisa huyo.
Leave a Reply