Mshukiwa mwingine wa Mungiki auawa kwenye msako wa wakazi – Taifa Leo


MSHUKIWA mwingine wa kundi haramu la Mungiki ameuawa kwa kukatwakatwa na nyumba yake kuchomwa moto huku wakazi wakiendelea kufukuza genge la wahalifu kutoka ardhi ya mradi wa makao wa Ngariama Kusini kaunti ya Kirinyaga.

Hii imeongeza idadi ya washukiwa wa kundi hilo ambao wameuawa katika muda wa siku tisa katika eneo hilo kuwa watatu.

Wakiwa na silaha butu, wakazi hao wapatao 500 walivamia nyumba ya mshukiwa huyo Alhamisi jioni eneo la Itangi na kumtoa nje.

Walidai yeye ni miongoni mwa wafuasi wa kundi hilo ambao wamekuwa wakichukua kwa nguvu sehemu ya mashamba ya wakazi hao..

Polisi walifika muda mfupi baada ya mauaji hayo na kupeleka mwili wa mshukiwa mochari ya hospitali ya Kerugoya.

Afisa mkuu wa polisi katika Kaunti Ndogo ya Mwea Mashariki Bw Mohammed Jarso alionya wakazi ambao wamekuwa wakishika doria katika eneo hilo dhidi ya kuua washukiwa.

“Inasikitisha mshukiwa aliuawa, hakuna haja ya kumwaga damu na wale wanaojihusisha na mauaji wanapaswa kuacha,’ alisema.

Alisema maisha ni matakatifu na yanafaa kulindwa, akiongeza kuwa maafisa wa usalama wanachukulia mauaji hayo kwa uzito.

Katika mauaji ya awali, washukiwa wawili walitolewa katika nyumba zao na kuchomwa moto.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*