Mswada kuweka sheria kali za kutoa viungo vya mwili wa binadamu – Taifa Leo


SHERIA mpya inayopendekezwa kujadiliwa na Bunge inaweka hatua kali za kuzuia utoaji na upandikizaji wa viungo vya binadamu.

Mswada wa Upandikizaji wa Viungo vya Binadamu 2024 unalenga kuunda mfumo wa kutoa udhibiti wa upandikizaji wa viungo vya binadamu na kuanzisha Mamlaka ya Upandikizaji wa Viungo vya mwili Kenya ambayo itadhibiti huduma zote zinazohusiana na sehemu za mwili wa binadamu na upandikizaji wa kiungo.

Sheria iliyopendekezwa ambayo kwa sasa inachunguzwa kabla ya kuchapishwa inafadhiliwa na Mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenje inakataza mtu kutoa, au kupokea zawadi au manufaa yoyote ya kiungo kilichotolewa kupandikizwa kutokana na matibabu ya ugonjwa.

Rasimu ya Mswada huo inasema kwamba viungo vya mtu aliyekufa vitaondolewa tu baada ya mhudumu wa afya kuthibitisha kuhusu kifo hicho.

“Kiungo cha binadamu kikitolewa kutoka kwa mwili wa marehemu, mhudumu wa afya atauchunguza binafsi mwili huo ili kuthibitisha kuwa uhai umetoweka katika mwili huo,” inasema rasimu ya Mswada huo.

Ingawa Mswada unaruhusu watu ambao bado wako hai kutoa viungo, hatua kama hiyo itafanywa tu kwa idhini ambayo lazima ifanywe kwa maandishi na pamoja na mashahidi wawili.

Kwa mujibu wa sheria iliyopendekezwa, kibali kitakuwa kwa njia ya maandishi na kutiwa saini na mtu anayekubali kuchangia mbele ya angalau mashahidi wawili wenye uwezo wa kufanya maamuzi.

Mswada pia unakataza kituo cha afya kutoa, kuhifadhi au kupandikiza tishu au kiungo cha binadamu kwa madhumuni ya matibabu isipokuwa kama kimesajiliwa ipasavyo.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*