ALIYEKUWA Balozi wa Kenya katika Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), Dkt Koki Muli anaonekana kutothaminiwa nyumbani licha ya kusaidia nchi nyingi za Afrika kuweka msingi bora katika mifumo yao ya uchaguzi.
Dkt Muli alijaribu kuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) mara tatu lakini hajafanikiwa licha ya uzoefu wake mkubwa.
Kwa sasa, Dkt Muli anakabiliwa na kikwazo kingine kutokana na mzozo ambao unaendelea kutokota katika kambi ya Azimio kuhusu mwakilishi wa muungano huo kwenye jopo la kuwapiga msasa makamishna wapya.
Nafasi hiyo imekuwa ikizozaniwa na Wiper ambayo imethamini Dkt Muli na chama cha NLP ambacho kimewasilisha jina la Augustus Muli ili ateuliwe katika jopo hilo.
Mtaala wa uchaguzi ambao aliuandika
Dkt Muli ndiye mwanamke pekee Afrika ambaye amehitimu kuwafundisha wanafunzi na kuwaidhinisha baada ya kumaliza masomo yao akitumia mtaala wa uchaguzi ambao aliuandika.
Iliyokuwa Tume ya Kriegler ambayo ilibuniwa kuchunguza ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, ilitambua juhudi na mafanikio yake.
Kati ya nchi ambazo zimefanikiwa kutumia mtaala wa demokrasia, uongozi na uchaguzi ulioandikwa na Dkt Muli ni Afrika Kusini, Botswana, Lesotho, Msumbiji, Zimbabwe, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uganda, Tanzania, Liberia, Ghana miongoni mwa mingine.
Nchini, Dkt Muli anaonekana kutokuwa na bahati kwenye jaribio lake mara tatu akitaka kuwa mkuu wa IEBC.
Mnamo 2009 alihojiwa ili ateuliwe mwenyekiti wa tume ambayo ingesimamia kura ya maamuzi ya 2010.
Cecil Miller aliteuliwa lakini jina lake likakataliwa na bunge. Miaka miwili baadaye Dkt Muli aliomba kazi hiyo lakini akapoteza kwa Isaack Hassan.
Kabla ya kuteuliwa kwa Bw Hassan majina ya Dkt Muli na Murshid Abdalla yalikuwa yamewasilishwa kwa aliyekuwa Rais Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.
Jopo la IEBC chini ya Aukot
Jopo la uteuzi wa mkuu mpya wa IEBC wakati huo liliongozwa na Dkt Ekuru Aukot.
Kama njia ya kumliwaza alipewa kazi ya kuwa naibu balozi wa Kenya kwenye Shirika la Umoja wa Kimataifa.
Hata hivyo, ilikisiwa kuwa alikosa kazi hiyo kwa kuwa alitoka kwenye kijiji cha karibu Kaunti ya Kitui na alikokuwa akitoka Jaji Mkuu wa wakati huo Willy Mutunga.
Kuelekea uchaguzi wa 2017, Dkt Koki alijaribu bahati yake tena lakini nafasi hiyo ikaendea Wafula Chebukati ambaye alimaliza muhula wake wa miaka sita.
Dkt Muli ni mkuu wa kitivo cha sheria katika Chuo Kikuu cha Southeastern Kenya na mzozo wa sasa unaonekana kushusha azma yake kwa kuwa hatawania kuwa mkuu wa IEBC bali kuwepo kwenye jopo la kuwapiga msasa makamishna na mwenyekiti mpya.
Katika mahojiano ya hapo awali, Dkt Muli alikataa mjadala kuhusu kuporomoka kwa azma yake mara tatu licha ya kuwa alionekana kuhitimu zaidi kuliko walioishia kukabidhiwa kazi hiyo.
Japo bahati haijasimama
Alisema kuwa japo bahati yake haijawahi kusimama, ataendelea kutumikia taifa lake.
“Hii ni nchi yangu na nina ari ya kuona kuwa uchaguzi mkuu unakuwa huru na haki. Kwa hivyo niko tayari iwapo nitaitwa kusaidia tume kuhakikisha hilo,” akasema.
“Si lazima nifanikiwe kuwa mkuu wa IEBC ila jambo muhimu ni kuwa anayeteuliwa anafahamu kazi anayoifanya, jinsi ya kuifanya na kupokea ushauri unaohitajika,” akaongeza.
Leave a Reply