Mtihani kwa ukuruba wa Ruto, Raila kufuatia pigo AUC na nyimbo za ‘Ruto Must Go’ Kondele – Taifa Leo


ITABIDI Rais William Ruto afikirie tena mikakati yake ya kupata wafuasi kutoka eneo la Luo Nyanza.

Hii ni baada ya Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kushindwa katika uchaguzi wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) Addis Ababa, Ethiopia.

Mshindi wa kinyang’anyiro cha Jumamosi ni Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Djibouti, Mahamoud Ali Youssouf.

Wachambuzi wa siasa wanasema ushindi wa Bw Odinga ungepiga jeki azma ya Dkt Ruto kuwania tena urais 2027.

Hii ni kwa sababu (Ruto) angekuwa mwaniaji mwenye nguvu zaidi wakati kiongozi wa upinzani hayupo kwenye ulingo wa siasa.

Tayari Kiongozi wa Taifa alikuwa anafurahia uungwaji mkono mkubwa sana kutoka kwa wakazi wa Nyanza hasa alipozuru eneo hilo.

Lakini baada ya Kenya kushindwa huko Addis Ababa, kelele za “Ruto Must Go” kwa maana ya “Ruto lazima aondoke (madarakani)” zilizuka Kondele, Kaunti ya Kisumu.

Wengine walimrai Bw Odinga aanze safari mpya ya kuwania urais kwa mara ya sita 2027 katika tukio linaloashiria kufifia kwa umaarufu wa serikali ya Kenya Kwanza eneo la Nyanza.

Ni hali ambayo inabashiriwa kuendelea kwa miezi kadhaa ijayo kama eneo la Mlima Kenya lilivyojitenga na Rais baada ya kutimuliwa kwa Rigathi Gachagua kutoka kwenye kiti cha naibu rais.

Juma lililopita, Seneta wa Siaya Oburu Oginga alidokeza kuwa chama cha ODM kinaweza kuwa na mgombeaji wa urais 2027. Tangazo hilo liliibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa chama cha Chungwa kumuunga mkono Rais Ruto atakapotafuta muhula wa pili Ikuluni.

Kulingana na Dkt Oginga, ambaye ni kaka yake Bw Odinga, kinara huyo wa ODM angali na uwezo wa kuwania urais.

“Tutakuwa na mgombeaji wetu wa urais kama ODM na iwapo kutakuwa na haja ya muungano na vyama vingine vyenye mawazo sawa, tutaamua mwaniaji bora pamoja. Lakini tutatoa uamuzi muda ukifika,” akasema.

Baada ya uchaguzi wa AUC, Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga alichapisha kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Facebook: ‘Baba, bado wewe ni Baba kila wakati’.

Baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wanaamini Bw Odinga hawezi kuwania urais kwa sababu ya umri wake wa miaka 80.

Afisa Mkuu wa Shirika la Kujadili Sheria la Asego (Asego Public Litigation Forum), Michael Kojo, anasema ni wakati aliyekuwa waziri mkuu ajiuzulu kisiasa.

“Kule Amerika, aliyekuwa Rais Joe Biden alimwachia aliyekuwa Naibu Rais Kamala Harris awanie urais kupitia chama cha Democratic kwa sababu yeye (Biden) amezeeka kiwango cha kuathiri kazi yake. Ninadhani Raila anafaa kumwachia mtu mchanga zaidi yake awe mgombeaji wa urais kupitia ODM,” akasema.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*