MCHEZAJI ghali kabisa kutoka Ukraine, Mykhaylo Mudryk, yuko hatarini kupigwa marufuku ya miaka minne kujihusisha na soka ikiwa itathibitishwa alitumia vidonge vya Meldonium kimakusudi.
Shirikisho la Soka Uingereza (FA) lilifahamisha klabu yake ya Chelsea kuwa sampuli ya kwanza ya mkojo wa Mudryk ilionyesha matumizi ya dawa hizo za Meldonium, ambazo Shirika la Kukabiliana na Matumizi ya Pufya Duniani (WADA) limepiga marufuku tangu mwaka 2016 kwa sababu zinaongeza nguvu ya ziada wanamichezo.
Winga huyo wa pembeni kushoto, anayepokea mshahara wa Sh16.4 milioni kila wiki (Sh853,387,600 kila mwaka) ugani Stamford Bridge, anadai kupatwa na mshangao baada ya kufeli vipimo hivyo.
Mudryk,23, ambaye anaaminika alikuwa akimezewa mate na miamba wa Ujerumani Bayern Munich, anaingia katika orodha ya wanamichezo waliopatikana watumiaji wa Meldonium iliyo na mwanatenisi Maria Sharapova (Urusi).
Wanasoka wengine tajika waliojipata pabaya ni pamoja na beki wa Ivory Coast Kolo Toure (miezi sita mwaka 2011 akiwa Manchester City), Mromania Adrian Mutu (miezi saba akiwa Chelsea mwaka 2004) na Paul Pogba (miezi 18 akiwa Juventus mwezi Februari 2024).
Mudyrk amepatikana pabaya wakati Chelsea wanafanya vizuri sana kwenye Ligi Kuu ya Uingereza. Blues wanakamata nafasi ya pili kwa alama 34, mbili nyuma ya viongozi Liverpool.
Raia huyo wa Ukraine tayari ametafuta huduma za mawakili waliosaidia Pogba kuona marufuku yake ya miaka minne ikipunguzwa hadi miezi 18.
“Nathibitisha kuwa nimearifiwa kuwa sampuli niliyowasilisha kwa FA ilikuwa na dawa zilizopigwa marufuku. Habari hizo zimenishangaza sana kwa sababu sijawahi kutumia dawa yoyote iliyopigwa marufuku kimakusudi ama kuvunja sheria zozote na ninashirikiana na timu yangu kuchunguza nini kilitendeka,” alitanguliza Mudryk kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.
“Najua sijafanya kosa na ninasalia mwingi wa matumaini kuwa nitarejea uwanjani hivi karibuni. Siwezi kusema zaidi ya hapo kwa sababu kesi inaendelea, lakini nitaweza kufanya hivyo itakapowezekana,” akasema.
Mudryk alijiunga na Chelsea kwa Sh9.4 bilioni (Yuro 70 milioni) kutoka Shakhtar Donetsk mnamo Januari 2023.
Imeandaliwa na GEOFFREY ANENE
Leave a Reply