MUME na mkewe wameshtakiwa kosa la kuiba Sh30.9 milioni kutoka chama cha akiba na mikopo.
Bw Francis Musau Musyimi na mkewe Bi Mercy Mbinya Muthoka pamoja na dada yake Charity Maua Muthoka wanazuiliwa katika korokoro ya kituo cha polisi cha Capitol Hill hadi Disemba 5, 2024.
Hiyo ni tarehe ambayo Hakimu Mkuu Ben Mark Ekhubi ataamua ikiwa wataaachiliwa kwa dhamana au la.
Wakati huo huo, Bw Ekhubi aliamuru polisi wamkamate Nicholas Muia Kyengo ambaye yuko mafichoni.
Hakimu alielezwa na kiongozi wa mashtaka Bi Virginia Kariuki kwamba Bw Musyimi alikamatwa katika mji wa Namanga akijaribu kutorokea Tanzania.
“Naomba hii mahakama itilie maanani kuwa Bw Musyimi alikamatwa akijaribu kutorokea Tanzania. Polisi walimtia nguvuni mjini Namanga,” Bi Kariuki akasema.
Musyimi, Mbinya na Maua walikana mashtaka sita ya kula njama ya kuiba na kutumia pesa za wizi kununua gari wakijua zimepatikana kwa njia isiyo halali.
Wanne hao wanashukiwa kuwa, kati ya Aprili 12, 2022 na Julai 18 2024, walikula njama kuiba Sh30,998,000 kutoka chama cha Progressive Credit Limited (PCL).
Musyimi na Kyengo, waliokuwa wafanyakazi wa PCL wameshtakiwa kwa kuiba kitita hicho cha pesa katika kipindi cha miaka miwili.
Mbinya ameshtakiwa pia kuiba pesa hizo naye dada yake (Maua) akashtakiwa kwa kosa la kuiba Sh15,499,000.
Musyimi na mkewe wameshtakiwa kwa kutumia pesa hizo zilizopatikana kwa njia ya uhalifu kununua gari muundo wa Toyota Caldina nambari ya usajili KBZ 083R.
Mahakama iliombwa iwazuilie watatu hao hadi Disemba 5, 2024 wahojiwe kwanza na maafisa wa urekebishaji tabia kubaini mienendo yao yao ya awali.
“Mtazuiliwa katika kituo cha polisi cha Capitol Hill muhojiwe na afisa wa urekebishaji tabia ndipo mahakama itathmini ombi lenu la dhamana,” Bw Ekhubi alisema.
Leave a Reply