WAZIRI wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, ametoa onyo kali kwa magenge ya wahalifu nchini huku akimwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, kuzima haraka shughuli zao.
Waziri Murkomen pia ameonya wanasiasa wanaofadhili au kufaidika na magenge hayo, akiahidi hatua za kisheria bila kujali hadhi yao. “Tumeona ongezeko la magenge ya wahalifu ambayo mara nyingi hufadhiliwa na wanasiasa kwa lengo la kutisha, kutesa, na kukandamiza wapinzani.
Wakiwa na silaha butu, magenge haya sasa ‘yanatoa ulinzi’ kwa viongozi huku yakitishia wapinzani kama ishara ya nguvu yao,” alisema Waziri Murkomen.
Agizo hili linatolewa huku umma ukilalamika kuhusu ongezeko la ukosefu wa usalama na ripoti za magenge haya kuvuruga shughuli za umma, ikiwemo tukio ambapo aliyekuwa kiongozi wa Mungiki, Maina Njenga, alivuruga mkutano huko Nyeri uliokuwa ukihudhuriwa na Pasta Dorcas Rigathi, mke wa aliyekuwa Naibu Rais-Rigathi Gachagua, na kumfanya kuondoka.
Magenge haya yanayoendesha shughuli zake Nairobi, Mombasa, Nakuru, Kiambu, Kisumu na maeneo mengine, yakihusika na uhalifu kama wizi, ulanguzi wa fedha, uhalifu wa mtandao na dawa za kulevya.
Makundi kama Mungiki, Confirm, Wakali Kwanza, na Sungu Sungu yalitajwa kwa shughuli zao hatari, kuanzia ulanguzi wa fedha, ushuru haramu, mauaji ya kikatili, hadi uporaji wa mashamba.
Akitoa mifano, Waziri Murkomen alielezea madhara yaliyosababishwa na Mungiki na Sungu Sungu hapo awali, ambayo yaliwaacha maelfu ya vijana maelfu wakiwa na majeraha, jamii zikiteseka, na imani ya umma kwa vyombo vya usalama ikapungua.
“Mauaji ya kutisha yaliyosababishwa na magenge ya Mungiki na Sungu Sungu ni onyo tosha la kutufanya tukomeshe magenge yoyote ya wahalifu mara moja kwa nguvu kubwa,” alisisitiza.
Leave a Reply