Mutahi Kagwe na Owalo wanusia uwaziri tena mabadiliko yakinukia – Taifa Leo


MABADILIKO yananukia katika Baraza la Mawaziri maelezo mapya yakionyesha kwamba Rais William Ruto anaweza kugawa wizara ya Barabara na Uchukuzi ili kushughulikia ushindani wa kisiasa huku akishauriana kwa mapana kuhusu wizara ya Masuala ya Ndani na Utawala wa Kitaifa.

Kwa kugawanya wizara inayoshikiliwa na Bw Davis Chirchir, Rais anasemekana pia kuwazia kuondoa wizara ya Jinsia na Utamaduni ili kutimiza hitaji la kifungu cha kikatiba cha ‘Mawaziri wasiopungua 14 na wasiozidi 22’.

Mawaziri walioteuliwa baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri mwezi Julai pia wanaweza kuhamishwa kutokana na ‘masuala ya utendakazi wao.’

Vidokezo ndani ya Ikulu vilisema kuwa idara ya Serikali ya Jinsia inaweza kuunganishwa na Wizara ya Utumishi wa Umma huku idara ya Utamaduni ikihamishiwa Wizara ya Utalii.

“Tulitarajia mabadiliko kufanyika mapema wiki iliyopita. Kuna uwezekano kwamba tangazo hilo litatolewa wakati wowote” duru za Ikulu zilisema.

Wizara ya Masuala ya Ndani na Utawala wa Kitaifa iliachwa wazi baada ya kupandishwa cheo kwa Prof Kithure Kindiki kuwa wa naibu rais.

Wizara ya Jinsia pia imekuwa wazi baada ya wabunge kumkataa Stella Soi, ambaye alikuwa ameteuliwa kushikilia wadhifa huo.

Bw Chirchir, mshirika wa karibu wa Rais Ruto, ndilo jina la hivi punde kutajwa kwa wadhida wa waziri wa usalama ya ndani. Bw Chirchir ni mshirika wa karibu wa Rais.

Alihamishwa kutoka wizara ya Kawi na Petroli hadi ya sasa wakati Rais alipounda Baraza la Mawaziri jumuishi.

Mbunge wa Belgut Nelson Koech, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kitaifa kuhusu Ulinzi, Ujasusi na Uhusiano wa Kigeni pia ametajwa kuwa anayeweza kuteuliwa kwa kusimamia wizara hiyo yenye nguvu.

Majina mengine ambayo yameibuka ya watu wanaoweza kuteuliwa kuhudumu katika Wizara hiyo ni Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, ambaye washirika wake walimtaka Rais waziwazi kumteua.

Kwa sasa Mudavadi ni kaimu waziri wa wizara hiyo.

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah pia ametajwa. Lakini Rais anasemekana kutoridhishwa na wazo la kumteua kiongozi yeyote aliyechaguliwa kutoka Mlima Kenya kwa kuwa inaweza kumpa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua jukwaa la kutanua misuli yake ya kisiasa katika uchaguzi mdogo.

Hata hivyo, baadhi ya viti vya uchaguzi viko wazi kwa sababu tume ya uchaguzi haijaundwa kusimamia chaguzi dogo za ubunge na wadi.

Eneo hilo kwa sasa linaonekana kuwa na chuki dhidi ya Rais Ruto kufuatia kutimuliwa kwa Bw Gachagua pamoja na hisia kuwa uongozi haujatekeleza ahadi zake za kabla ya uchaguzi mkuu.

Pia waziri wa Mazingira Aden Duale anasemekana kumezea mate wadhifa huo. Bw Duale alihamishwa kutoka wizara ya Ulinzi hadi wizara ya sasa na ni miongoni mwa washirika wa karibu wa Rais waliojiuzulu viti vya Ubunge na kujiunga na serikali.

Duru za Ikulu zinaonyesha kuwa Rais Ruto ana nia ya kuepuka kuwa na Baraza la Usalama la Kitaifa lenye watu wa kabila moja.

Kifungu cha 240 cha katiba kinaunda Baraza la Usalama la Kitaifa, likijumuisha Rais, Naibu Rais, mawaziri wanaosimamia Ulinzi, Masuala ya Kigeni na Usalama wa Ndani, pamoja na Mwanasheria Mkuu, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi.

Wanachama wa sasa wa baraza hilo ni pamoja na; Rais Ruto, Naibu Rais Kindiki, Waziri wa Ulinzi Soipan Tuya, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi anayesimamia Masuala ya Kigeni na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor. Wengine ni Mkuu wa Majeshi Charles Kahariri, Mkurugenzi Mkuu wa NIS Noordin Haji na Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja.

Huku tayari wanachama watatu wa baraza hilo wakitokea eneo la Mlima Kenya, inasemekana kuna uwezekano wa Rais Ruto kukabidhi wadhifa eneo tofauti.

Vyanzo vya habari vilidokeza kuwa Rais alikuwa akiwazia kuteua mshirika wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kwenye Baraza lake la Mawaziri.

Aliyekuwa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe ametajwa kuwa miongoni mwa wanaowaziwa kujiunga na Baraza la Mawaziri.

Bw Kagwe, na Naibu Mkuu wa Wafanyakazi katika Ikulu anayehusika na Utendaji na Usimamizi wa miradi Serikalini, Bw Eliud Owalo wametajwa kuwa watu wanaoweza kuteuliwa kuchukua wizara ya Uchukuzi na Barabara, endapo itagawanywa.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*