Mvutano mpya wazuka kuhusu mali ya Nyachae – Taifa Leo


UUZAJI wa mali inayohusishwa na kampuni moja iliyoanzishwa na aliyekuwa mwanasiasa na mfanyabiashara Simeon Nyachae umezua mzozo mpya miongoni mwa watoto wake.

Katika kesi iliyo mbele ya Mahakama Kuu ya Milimani, mmoja wa ndugu hao aliomba kibali cha mahakama kushtaki kwa niaba ya Kampuni ya Sansora Bakers & Confectioneries Limited na kampuni mlezi Sansora Investment Ltd.

Chanzo cha mzozo huo ni uuzaji wa mali katika Kaunti ya Kisii ambayo ilidaiwa kuuzwa kwa Sh8 milioni lakini ingefaa kuuzwa kwa zaidi ya Sh35 milioni.

Kupitia kwa wakili Simon Njege, ndugu hao wamewashutumu wakurugenzi wa kampuni hiyo Michael Moragia Nyachae na Jamaludin Shamsudin Alibhai kwa kuendesha kampuni kama mali ya kibinafsi na kuwatenga wenyehisa wake.

“Kutokana na ukiukaji uliotokana na washtakiwa, kampuni iko katika hali ya hatari kwani kuendelea kusimamiwa vibaya kunaiweka katika hatari zaidi na hasara isiyoweza kurekebishwa kwa wenyehisa wake,” Bw Njege alisema katika kesi hiyo.

Bw Nyachae alifariki Mei 1, 2021 na wanawe wanavutana kuhusu urithi baada ya Bi Margaret Kerubo Chweya, kutaka kujiunga na kesi hiyo akidai kuwa mke wa Nyachae na kutaka agawiwe hisa za mali hiyo.

Uuzaji wa jengo hilo mnamo Mei 2021 umepingwa kwa sababu ya mgongano wa masilahi kwa sababu wakurugenzi wameweka masilahi yao ya kibinafsi mbele ya kampuni.

Aidha wakurugenzi hao wanadaiwa kushindwa kufanya kazi kwa nia njema katika kukuza mafanikio ya muda mrefu ya kampuni hiyo kwa manufaa ya wenyehisa wote.

Miongoni mwa maagizo ikiwa kesi hiyo itafaulu, ni kuwashurutisha wakurugenzi watoe vitabu vya akaunti, taarifa ya benki kuhusu mauzo ya mali hiyo, taarifa za fedha zilizokaguliwa na taarifa za benki za Sansora Bakers & Confectioneries kuanzia 2021 hadi sasa.

Inadaiwa kuwa kampuni hiyo inaendeshwa kwa siri na wakurugenzi hao ambao hadi leo walishindwa kutoa taarifa muhimu kuhusiana na mali hiyo ikiwa ni pamoja na makubaliano ya mauzo.

Mahakama Kuu ilitoa amri ya muda dhidi ya kuuza au kuhamisha Sansora Bakery & Confectionary Ltd, kusubiri kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Akijibu, Bw Moragia alisema kuwa kampuni ya kutengeneza mikate ilikuwa mojawapo ya kampuni zilizoanzishwa na marehemu Nyachae na kwamba ilikuwa desturi yake kuwekeza fedha za ziada katika mali kwa maendeleo ya baadaye.

“Tangu kuanzishwa kwa mlalamishi wa 2 (Sansora Bakers & Confectionery ltd), biashara imefanya kazi bila maazimio ya maandishi – wakurugenzi, ambao wamejumuisha marehemu baba yangu, kwa muda wote wamekuwa wakifanya kazi kwa nia njema, kulingana na mahitaji ya kampuni,” alisema.

Alisema wakati wowote ikihitajika, marehemu Nyachae, Bw Alibhai na yeye walikuwa wakikubaliana kwa mdomo, kutoa baadhi ya mali na kuwekeza fedha hizo tena.

Kwa upande wake, Bw Alibhai alisema maagizo ya kufunga akaunti za benki za kampuni hiyo yalifanya iwe vigumu kuendeleza shughuli zake.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*