Mwaka wa 2024 umekuwa wa mafanikio makubwa kwa Kiswahili – Taifa Leo


MWAKA wa 2024 umekuwa wa mafanikio makubwa kwa Kiswahili. Mnamo Machi, Serikali ya Uganda ilitenga Dola milioni 800 za Kimarekani kwa kusudi la kukuza na kufunza Kiswahili. Taarifa hii ilitolewa na Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki, Bi Rebecca Kadaga.

Bi Kadaga alieleza kuwa watumishi wa umma wangepewa nafasi ya mwanzo kujifunza Kiswahili. Aliongeza kuwa serikali ilipania kueneza matumizi ya Kiswahili na kwa hivyo maafisa wote wa ngazi ya juu serikalini walikuwa wakipokea mafunzo ya Kiswahili.

Nchini Kenya, Taasisi ya Ukuzaji Mitaala (KICD) ilitangaza Kiswahili kama somo la lazima na la kutahiniwa kuanzia gredi ya kwanza hadi ya tisa. Jambo hili linahakikisha kuwa kila mtoto wa Kenya anayeingia shuleni anapata uelewa wa wastani wa Kiswahili.

Kiswahili pia ni somo la lazima kwa wanafunzi wanaoteua mkondo wa sayansi za kijamii, kitengo cha lugha na fasihi. Ikumbukwe pia kwamba mswada wa kuunda Baraza la Kiswahili ulipita hatua ya kwanza bungeni bila kupingwa.

Baadaye, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) lilipitisha Azimio (A/78/L.83) lililotenga Julai 7 kuwa Siku ya Kiswahili Duniani (SIKIDU). Azimio hilo pia lilipita bila kupingwa.

Hatimaye, mwezi uliopita, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inayoshirikisha nchi nane wanachama ilipitisha kauli kuwa Kiswahili kiwe mojawapo ya lugha tatu rasmi za Jumuiya. Uamuzi huu utasaidia sana katika makuzi na maenezi ya Kiswahili.

Matukio haya ndiyo yanayotufanya kusema kuwa huu wa 2024 umekuwa mzuri kwa Kiswahili. Mambo yakiendelea kwa kasi hii mwakani, basi mustakabali wa Kiswahili utakuwa mzuri sana.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*