Mwalimu mwingine wa Kenya ateuliwa kuwania tuzo ya mwalimu bora duniani baada ya Peter Tabichi – Taifa Leo


MIAKA sita tangu mwalimu Peter Tabichi kushinda tuzo ya mwalimu bora duniani, mwalimu mwingine kutoka nchini Kenya ameteuliwa kuwania tuzo hiyo ya hadhi.

Bw Dominic Orina, ambaye ni mwalimu wa kilimo katika Shule ya Msingi ya Kugerwet, inayopatikana katika eneobunge la Konoin, katika kaunti ya Bomet ni miongoni mwa walimu 50 wa mwisho katika uteuzi huo.

Mshindi wa tuzo hiyo iliyoanzishwa miaka minane iliyopita, hukirimiwa Sh129 milioni kutokana na ubunifu wao ambao huchangia kwa njia za kipekee katika kazi yao.

Akiongea na Taifa Leo baada ya uteuzi wake, Bw Orina aliwataka Wakenya kumuombea ili aibuke mshindi.

“Ndugu zangu Wakenya, nitilie dua ili niitwae zawadi hii. Ikiwa nitatangazwa mshindi, ushindi wangu hautakuwa wangu pekee bali kwa nchi yetu nzima,” Orina alisema.

Tangu alipoajiriwa katika Shule ya Kugerwet mwaka 2017, Bw Orina aliwaongoza wanafunzi wake kuanzisha mradi wa ukuzaji mboga na ufugaji sungura. Alifanikisha hili kufuatia ufufuzi wa chama cha 4K shuleni humo.

Kutokana na kauli mbiu ya chama hicho ya Kuungana, Kufanya na Kusaidia Kenya, mwalimu huyo amefanikiwa kuwajenga wanafunzi hao kuwa na moyo wa kujitegemea na kuzalisha mboga kwa wingi kwa matumizi yao shuleni na nyumbani.

Bw Orina ambaye ni mzawa wa kaunti ya Nyamira, anafahamika sana mitandaoni kutokana na kazi yake ya kukuza mboga kwenye magunia na karatasi za plastiki.

Mwaka 2020, mwalimu mwingine wa Kenya Linah Anyango naye alikuwa miongoni mwa washindani wengine 50 walioteuliwa kuwania taji hiyo.

Bw Orina vilevile, amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kuwarai wahisani kuwanunulia sare baadhi ya wanafunzi wake wanaotoka katika familia zisizojiweza.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*