MWANACHUO Mtanzania amejitoa uhai katika bweni moja wanamoishi wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amerika (USIU), bewa la Nairobi.
Kulingana na ripoti kutoka kituo cha Polisi cha Kasarani, Jumatano, Novemba 4, 2023, inashukiwa kuwa Benedict Mberesero, 21, alijiua kwa kuruka kutoka orofa ya 11 ya jengo kwa jina, Abardare Heights kuliko bweni hilo.
“Meneja wa Usalama katika Qwetu USIU 4 Bi Rachael Thogori aliripoti kwamba alifahamishwa na wafanyakazi wake kwamba leo Desemba 4, 2024, mwendo wa saa kumi na nusu alfajiri, katika bweni la Qwetu, lililoko Abardare Heights……….. mkazi kwa jina Benect Mberesero, raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 21 anashukiwa kujiua kwa kuruka kutoka paa la jengo hilo lenye orofa kumi na moja,” taarifa hiyo ikasema.
Kulingana na polisi, mwili wa marehemu ulipatikana sakafuni karibu na lango kuu la jengo hilo.
“Mikono na miguu ilikuwa imevunjika sawa na fuvu la kichwa. Ilibainika kuwa mwendazake alikuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha USIU,” taarifa ya polisi ikaeleza.
Maafisa wa polisi kutoka kituo cha Kasarani, waliofika eneo la tukio, walipata nyaraka nne chumbani mwa marehemu ambazo aliwaandikia mamake, kakake na dadake.
Aidha, ilibainika kuwa Mberesero aliacha kwenye la jengo hilo, simu yake, viatu na kadi ya kufungulia mlango wa chumba chake.
Mwili wa mwendazake ulipelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTTRH) kusubiri kufanyiwa upasuaji.
Polisi walisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha tukio hilo.
Visa vya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Kenya kujitoa uhai vimekuwa vikiripotiwa kwa wingi katika siku za hivi karibuni.
Wataalamu wanasema visa hivyo vinachangiwa pakubwa na changamoto za kijamii, kifedha na matumizi mabaya ya pombe na mihadarati.
Kwa mfano, mnamo Oktoba 21, mwaka huu mwili wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi kwa jina Frankine Ondwari, 27, alipatikana ndani ya choo moja katika barabara ya Kirinyaga Road. Uchunguzi wa polisi ulibaini kuwa mwanafunzi huyo alijiua.
Leave a Reply