Mwanamke afariki baada ya kuumwa na nyoka wa pasta – Taifa Leo


FAMILIA moja katika Kaunti ya Busia inaomboleza mama yao aliyefariki baada ya kuumwa na nyoka wa pasta aliyekuwa akiombea jirani yao.

Mnamo Alhamisi alasiri, Bi Margaret Agutu aliungana na majirani zake katika kijiji cha Murende, Kaunti-ndogo ya Matayos, Busia kushuhudia miujiza ambayo ilifanywa na ‘pasta’ mmoja katika boma moja la jirani yake kwa madai kwamba alikuwa mchawi.

Hakujua kwamba angeumwa na ‘nyoka wa pasta’ na yeye kubadilika kuwa muujiza uliokusudiwa. Familia yake imebaki na maswali mengi yasiyo na majibu baada ya ‘kipindi cha maombi’ kilichohusisha matumizi ya nyoka kugeuka msiba baada ya kuumwa na nyoka huyo na kufariki dunia.

pasta feki

Mume wa marehemu, Alloyce Ouma Okumu alisema mkewe alikuwa amehudhuria ‘maombi’ yaliyoongozwa na ‘pasta feki’ ambaye anadaiwa kufanya miujiza katika boma la jirani yao kwa kutumia zana za kustaajabisha, miongoni mwao nyoka.“Wakati wa maombi hayo, nyoka aliibuka na ndipo watu wakaanza kukimbilia usalama wao.

Mke wangu alianguka chini na kukanyagwa na watu wengine watatu ambao walishtuka kumuona yule nyoka. “Nyoka alimuuma mke wangu kwenye kidole chake kimoja,” akaeleza Bw Okumu.

Alisema kilio cha mkewe kwa kung’atwa na nyoka huyo kilipuuzwa na ‘pasta’ huyo ambaye aliendelea na ‘maombi’ yake huku hali yake ikizidi kuwa mbaya.

‘Pasta alipogundua kuwa hali ya mke wangu ilikuwa mbaya, alimchukua nyoka, na kumweka kwenye gunia pamoja na zana zake nyingine za kushangaza za kazi, na katika hali ya kushangaza, akatoroka,’ akasema.

Mwanamke huyo alifariki baada ya kuumwa na nyoka mwenye sumu alipokuwa akikimbizwa hospitalini. Madaktari walisema mwanamke huyo alionekana kuzidiwa na uchungu kwa sababu nyoka huyo alikuwa na sumu kali.

Moyo kwenda mbio

Dk Donald Musi wa Hospitali ya Plateau alisema mtu aliyeumwa na nyoka hupata dalili za moyo kwenda mbio na kuzirai.

“Iwapo mtu ameumwa na nyoka, ni muhimu atulie. Kutembea kunaweza kusababisha sumu kupita haraka mwilini na kusababisha kutokwa na damu, figo kushindwa kufanya kazi na wakati mwingine kupata matatizo ya kupumua na kifo.

“Huduma ya matibabu ya dharura inafaa kupatikana haraka iwezekanavyo,” akasema Dkt Musi.Visa vya mapasta feki kusababisha vifo vinaendelea kukithiri nchini huku serikali ikishinikiza makanisa na wahubiri wadhibitiwe.

Baadhi yao wanahubiri wakiwa na nyoka ili kufanya miujiza na kuthibitisha uwezo wa Yesu Kristo ndani yao.

Wakazi wa kijiji cha Murende wameomba maafisa wa usalama kuanzisha uchunguzi wa kina ili kumkamata ‘pasta’ aliyetoroka.Bw Stella Athieno, binti wa marehemu alisema ili familia ipate haki, lazima mtu huyo akamatwe na kushtakiwa.

“Kwa nini pasta atumie nyoka mwenye sumu kali kwenye kipindi cha maombi ikiwa nia si kuwafumba macho wafuasi wake. Wachungaji kama hao wana mazoea mabaya na ni lazima wazuiwe kufanya shughuli hizo hatari,” akalalamika Bi Athieno.

Msaada wa kifedha

Familia hiyo pia imeomba usaidizi wa kifedha kugharimia ada za kuhifadhi maiti na mazishi ikidai maafa yaliwakumba kipindi hiki kigumu kiuchumi.“Mapasta hao wamekuwa wakitumia udhaifu wa kiroho wa waumini kuishi maisha ya kidhania.

Wachungaji kama hao wana mazoea ya kustaajabisha, na ni lazima wazuiwe kufanya shughuli zao hizo” akalalamika Bi Athieno.

Familia hiyo pia imeomba usaidizi wa kifedha kugharimia chumba cha kuhifadhia maiti na mazishi ikidai maafa yaliiikumba wakati huu ambapo hali yake ya kifedha ni duni. Mwili wa marehemu ulipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Rufaa ya Busia.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*