
MWANAMUME mwenye umri wa miaka 42 kutoka kijiji cha Kilimani, Likuyani kaunti ya Kakamega Jumanne usiku alimuua kakake wakizozania ugali.
Bw Reuben Lutaboni alidaiwa kumuua kakake Michael Lukala, 40, kwa kutumia shoka baada ya kutofautiana kuhusu kiasi cha ugali waliokuwa wakitayarisha jikoni kwa mama yao.
Wawili hao walikuwa wameshinda mchana wakichimba kisima cha maji kwa jirani yao kabla ya kurudi nyumbani wakiwa na njaa na uchovu.
Waliingia jikoni kwa mama yao ili kuandaa ugali na omena lakini Lukala hakujua kuwa ugali waliokuwa wakiuandaa ungekuwa wake wa mwisho.
Kulingana na Peter Lukala, kaka yao mkubwa, ndugu hao wawili walirejea nyumbani jioni ili kuandaa chakula chao kabla ya mzozo kuzuka na kusababisha kifo cha kikatili cha Michael Lukala.
“Kulizuka mabishano makali walipokuwa wakipika ugali yaliyosababisha vita vilivyokatiza maisha ya kaka yetu mdogo,” akasimulia Bw Peter Lukala.
“Michael na Reuben walikuwa marafiki wazuri sana. Walikuwa wakitafuta vibarua na kuvifanya pamoja. Sielewi ni nini kiliwapata hadi wakagombana na kupigana,” Lukala aliongeza.
Bi Esther Akwam, mama yao alieleza kuwa Reuben alimuua kakake kwa kutumia shoka.
“Alishika shoka na kumvamia Michael kutoka nyuma, na kumpiga mara kadhaa kichwani. Alikufa papo hapo,” alisimulia.
Alisema alijaribu sana kuingilia kati kusitisha vita hilo lakini alizidiwa nguvu na kuwatazama wanawe wakipigana hadi mmoja akafariki
“Niliwasikia wakigombana na nikakimbia kuona kilichokuwa kikiendelea. Niliwakuta wakipigana na nikajaribu kuwatenganisha, lakini walinishinda nguvu. Nilipiga kelele kuwaita majirani zetu ambao walifika kuchelewa. Michael alikuwa amelala sakafuni kwenye dimbwi la damu akiwa amekufa,” alisimulia.
Majirani wamemlaani mwanamume huyo kwa kumuua nduguye kwa sababu ya ugali
Bw Cleophas Barasa, mzee katika kijiji alizitaka familia kutumia njia za amani kusuluhisha mizozo.
“Inasikitisha kwamba ugomvi mdogo kuhusu ugali unaweza kuishia katika hasara hiyo ya kusikitisha. Ni lazima watu wajifunze kusuluhisha mizozo yao bila vita,” alisema.
Leave a Reply