![DNOTIENOREQUEUMMASS0502a-1320x792.jpg](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2025/02/DNOTIENOREQUEUMMASS0502a-1320x792-678x381.jpg)
MWANAHARAKATI wa Molo, Richard Otieno aliyeuawa mwezi jana atazikwa Ijumaa, Februari 7, 2025 huku maafisa wa upelelezi wakiendelea kuwasaka waliomuua kinyama.
Huku miito ikitawala ikitaka uchunguzi kuhusu mauaji hayo ufanywe, Taifa Leo imebaini kuwa mwanasiasa mwenye ushawishi anahusishwa na suala hilo.
“Tumeomba data kutoka kwa Safaricom ili tuweze kufuatilia mawasiliano. Mwanasiasa huyo ataandikisha taarifa wiki ijayo. Pia tunafuatilia vitisho ambavyo mwendazake alipokea kabla ya kuuawa na watu ambao walikuwa wakimfuata,” akasema afisa mmoja wa upelelezi anayehusika katika uchunguzi huo.
“Katika siku zijazo, huenda tukawakamata washukiwa zaidi kuhusiana na mauaji hayo,” akaongeza mpelelezi huyo. Jumla ya watu saba, wakiwemo watu wa familia ya Otieno, wameandikisha taarifa kuhusu mauaji hayo.
Maafisa wa upelelezi wanasema wamekusanya maelezo zaidi yatakayowawezesha kuwakamata washukiwa zaidi wa mauaji ya Otieno, 33, aliyefahamika eneo la Molo kama ‘Molo President’.
Kulingana na familia yake Otieno, maiti yake itazikwa nyumbani kwa wazazi wake Kaunti ya Siaya.
Mwendazake, aliyekuwa kiongozi wa vijana na mkosoaji mkuu wa serikali na Mbunge wa Molo Kuria Kimani, aliuawa Januari 18 umbali wa mita chache kutoka kituo cha polisi cha Elburgon.
Mnamo Jumatano, miito ya kutaka haki ipatikane ilishamiri wakati wa ibada ya wafu ya Otieno katika Kanisa Katoliki la St Peter’s mjini Elburgon.
Viongozi wa eneo hilo walishinikiza uchunguzi wa kina ufanywe ili waliotekeleza mauaji hayo ya kinyama wakamatwe na kushtakiwa.
Ingawa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wamewakamata washukiwa watano kuhusiana na mauaji hayo, viongozi wa eneo hilo walitaka wadhamini wa uhalifu huo ndio wakamatwe.
Leave a Reply