Mwangaza asema afueni ya kudumu ofisini muda zaidi ni zawadi ya Krismasi – Taifa Leo


GAVANA Kawira Mwangaza wa Meru ametaja uamuzi wa kuongeza muda agizo linalozuia kuondolewa kwake ofisini, kama zawadi bora zaidi ya Krismasi.

Katika uamuzi uliotolewa Jumatano, Jaji Bahati Mwamuye aliongeza muda wa agizo hilo kwa siku 120 akitaja maslahi ya umma kama sababu ya kufanya hivyo.

Jaji alisema kutoongeza muda wa agizo hilo, huku kesi ya gavana bado ikiendelea, kunamaanisha kuwa wadhifa wa gavana wa Meru utajazwa.

“Mabadiliko hayo hayatakuwa rahisi kuyafuta iwapo kesi ya gavana itafaulu,” alisema Jaji.

Gavana Kawira Mwangaza katika Mahakama Kuu ya Milimani mnamo Oktoba 8, 2024, wakati wa kusikizwa kwa kesi anayopinga kutimuliwa kwake ofisini. PICHA | WILFRED NYANGARESI

Maseneta waliidhinisha uamuzi wa Bunge la Kaunti ya Meru kumtimua Bi Kawira mnamo Agosti 21, baada ya jaribio la tatu la kumuondoa.

Maseneta 26 walipiga kura kuunga mkono mashtaka matatu dhidi ya Bi Mwangaza.

Hata hivyo alifika mahakamani siku hiyo hiyo na Jaji Mwamuye akasimamisha utekelezaji wa uamuzi wa Bunge na kumuondoa ofisini.

Seneti ilikuwa imeitaka mahakama kutupilia mbali agizo hilo, ikidai linaingilia mamlaka ya bunge hilo.

Seneti pia ilimlaumu Bi Mwangaza, ikisema alifaa kushtaki Seneti wala si spika.

“Mlalamishi ataendelea kuhudumu kama gavana kwa kufahamu kwamba hukumu katika kesi hii inaweza kutolewa kabla ya kukamilika kwa siku 120,” alisema Jaji Mwamuye.

Gavana Mwangaza mbele ya Seneti wakati wa vikao vya kujadili hoja iliyopitishwa na Bunge la Meru kumtimua mamlakani, mnamo Agosti 19, 2024. PICHA | DENNIS ONSONGO

Alisema Bi Mwangaza alidhihirishia mahakama kuwa kesi hiyo haitakuwa na maana ikiwa amri ya muda ya kuzuia kuondolewa kwake ingeondolewa ilivyoomba Seneti.

Bi Mwangaza alishindwa kuzuia machozi jaji alipoongeza muda wa agizo la kuzuia kutimuliwa kwake.

“Kile ambacho Mungu amekupa hakuna mtu anayeweza kukiondoa, hata baada ya siku 120 kiti bado kitakuwa changu,” Bi Mwangaza alisema.

Wakili Mugambi Imanyara alisema uamuzi huo ni zawadi bora zaidi ya Krismasi kwa watu wa Meru.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*