Mzee hafai kunywa maziwa ya mtoto ila hapa Kenya wabunge wanahepesha visenti vya walinzi wao – Taifa Leo


DAH! Mwaka mpya umesalia siku 29 pekee. Siku zinazonga kweli. Labda umeanza kuandika maazimio ya mwaka mpya, ila nina hakika hujatekeleza hata nusu ya maazimo ya mwaka huu. Karibuni ‘utakula’ Krismasi na Jamhuri. Sherehe zimefika!

Naambiwa waliokuwa na mipango mahsusi ya kupunguza uzito wameisitisha kati ya sasa na mwisho wa mwaka ili wale bata, watafune vya kutafunwa na kupiga mafunda ya vinywaji wavipendavyo. Msisimko wa sikukuu umeingia, hata kazini hatutaki kwenda!

Nimejihesabu pia kwa sababu ningali binadamu, napenda kupiga sherehe. Hata hivyo, kuna kitu kimoja ambacho sijawahi, na sitawahi, kufanya: Kuandika maazimio ya mwaka mpya.

Naongozwa na maadili haya

Maishani naongozwa na maadili haya: Fisi hamli mwanawe, baba hanywi maziwa ya mtoto, achana na ukoko ikiwa umefikiwa na tonge la ugali, usiibie omba-omba, hasa akiwa kipofu, na usikalie tawi unalokata.

Mbunge wako unayependa kuita mheshimiwa hajui maadili haya, ndio maana amekuwa akiiba posho za kila siku za dereva na mlinzi wao, watu wawili muhimu zaidi katika maisha yake.

Hebu tafakari yule mbunge wako akiwaibia tarishi na dereva wake Sh4,200 ambazo wao hulipwa wakiandamana naye katika shughuli rasmi zisizowaruhusu wasaidizi hao kulala kwenye nyumba zao.

Ikiwa mbunge anaiba hela kidogo hivyo, unadhani mamilioni yako ya maendeleo mashinani (CDF) yatasazwa? Ukubwa wa mlo humtamanisha mlaji akataka kuendelea.

Ukimwibia mlinzi wako

Huhitajiki kuwa na akili nyingi ili kujua kuwa ukimwibia mlinzi wako, hasa ikiwa yeye hutumia silaha kukuweka salama, kuzimu kunakuita! Ni sawa na kulala mlango wazi, ukafunga macho na kuamini mwizi akikuvamia usiku hatakuona.

Ikiwa una akili razini, huwezi kumwibia mtu ambaye hushika usukani wa chombo unachosafiria! Je, njaa ikizidi, minyoo ilalamike, tumbo limsokote, azame kwenye bahari ya luja na kupita na nguzo zilizo za barabara?

Sawa na Papa wa Roma alivyowauliza wabunge hivi majuzi, unawezaje kumwibia msaidizi wako wa msingi kabisa Sh4,200 ilhali unalipwa shilingi zaidi ya milioni moja kila mwezi? Kwani lako ni tumbo lisiloshiba? Unataka ngapi ndio uache wizi uchwara?

Wanasiasa wengi nchini Kenya wana hulka ya kutembelea kizani wanapopanga mikakati haramu ya kujitajirisha, na huko-huko kizani wanapitia na wasaidizi wao.

Hivi unapomwibia mtu anayezijua siri zako zote, unamuona mjinga asiyeelewa kitu, mwoga asiyethubutu kusimulia ya kwako, au hujali anavyohisi?

Wapaswa kuunda kundi la WhatsApp

Madereva na walinzi wa wabunge ambao huiba pesa hizo wanapaswa kuunda kikundi cha WhatsApp ili wajitafutie suluhisho la kudumu, pesa zao zianze kuingia kwenye akaunti zao mara moja.

Na wasifiche ukweli kwamba wana kikundi hicho, mwanzo wakijadili wakubwa wao hapo wapige picha na kutuwekea mitandaoni ili sote, pamoja na wake za wakubwa hao, tujue nyumba ndogo zimefichwa wapi!

Lazima tuikarabati nchi hii kwa sababu Zakayo ameshindwa.

[email protected]



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*