NAIBU wa Msajili Mahakama ya Leba Joseph Kaverenge amefungwa jela siku saba kwa kukaidi agizo la Mahakama Kuu kwamba afikishe kortini Sh13.5milioni zilizopatikana na mfanya biashara aliyeshtakiwa kuiba (KSh140milioni) miaka mitano iliyopita mjini Dubai.
Bw Kaverenge alisukumwa jela na Jaji Alexander Muteti alipokosa kuwasilisha pesa hizo alizodai zimewekwa ndani ya sefu ya Mahakama Kuu na kifunguo kiko na afisa aliye likizoni.
Pesa hizo zilitwaliwa na polisi kutoka kwa Rebecca Mueni Musau aliyeshtakiwa pamoja na George Gitau Maina kwa wizi wa KSh140 milioni.
Mueni na Gitau walidaiwa kuiba pesa hizo kutoka kampuni ya Transguard Company mnamo Machi 4,2018 katika duka kwa jina Deira City Centre Mall (UAE).
Mueni na Gitau walitoroka Dubai kisha wakatiwa nguvuni Machi 2018 na Novemba 2018 mtawalia.
Polisi walimpata Mueni akiwa na Sh13.3milioni katika eneo la Kamulu kaunti ya Machakos naye Gitau akiwa na Sh240,000 katika eneo la Mwihoko kaunti ya Kiambu.
Naibu msajili huyo aliomba apewe muda hadi Januari 13,2025 wakati afisa aliye na kifunguo atakapotoka likizoni ndipo aweze kuchukua pesa hizo awasilishe kortini.
Hata hivyo Jaji Muteti hakusikiza kilio cha Bw Kiverenge na akaamuru apelekwe gerezani hadi Januari 13,2025 atakaporudishwa kortini kwa maagizo zaidi.
Jaji huyo alisema ripoti ya awali inaonyesha Bw Kiverenge hakuwasilisha fedha hizo kukaguliwa na kuhesabiwa tena kubaini kama Sh13,540,000 zingali zote.
Mnamo Desemba 31 2024 Bw Kiverenge alipewa muda hadi Januari 3,2025 afikishe pesa hizo kortini.
Lakini hakuzileta pesa ndipo mawakili Ishmael Nyaribo na Thomas Mbaka wakaomba Jaji Muteti amwadhibu naibu msajili huyo.
Kabla ya kuhukumiwa Bw Kiverenge alihakikishia Jaji Muteti kwamba pesa hizo zipo na ufunguo wa sefu ambapo pesa hizo zipo una afisa aliye likizoni.
“Naomba hii mahakama inipe muda hadi Januari 13,2025 afisa anayehifadhi ufunguo arejee kazini kutoka likizoni,” wakili Stanley Kang’ahi anayemwakilisha Bw Kiverenge alieleza mahakama.
Ombilo halikukubaliwa kisha Jaji Muteti akaamuru Bw Kiverenge apelekwe jela hadi Januari 13,2025 atakaporudishwa kortini kwa maagizo zaidi.
Leave a Reply