KWA kila kilo moja ya miraa inayosafirishwa hadi Somalia kwa ndege, kundi linaloaminika kuungwa mkono na serikali hulipwa Sh581.89.
Hii ina maana kuwa linapokea zaidi ya Sh10 milioni kwa siku kwani Kenya husafirisha nje takriban tani 20 za miraa kila siku.
Ukusanyaji wa ada katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) umekuwa ukiendelea tangu Julai 2022 wakati aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia Hassan Mohamud walipotia saini mkataba uliofuta marufuku ya miaka miwili ya kuuza miraa nje ya nchi.
Katika mpango huo, kiasi cha miraa iliyosafirishwa kwenda Mogadishu kilipunguzwa hadi tani 20 kwa siku kutoka zaidi ya tani 50 zilizokuwa zikiuzwa kabla ya Covid-19.
Imeibuka kuwa mbali na serikali ya Somalia kuweka kiwango cha kila siku cha tani 20 kwa miraa ya Kenya, wauzaji nje walitakiwa kulipa Sh581.89 kwa kilo kabla ya mizigo yao kuondoka Kenya.
Hata hivyo, ushuru huu haukuwa katika makubaliano yoyote ya biashara kabla ya mauzo ya nje kuanza tena.
Kulingana na afisa mmoja aliyekuwa akifanya kazi katika wizara ya Kilimo wakati huo, ‘ada’ hiyo ilikubaliwa kati ya maafisa wakuu wa serikali kutoka pande zote mbili.
“Pesa hizo zinakwenda kwa maafisa wenye nguvu sana. Wanakusanya mamilioni ya pesa kila siku kwa gharama ya wakulima wa miraa,” alisema kwa sharti la kutotajwa jina.
Mnamo 2022, Chama cha Wafanyabiashara wa Miraa cha Nyambene (Nyamita) kilizua hofu kuhusu jinsi ushuru huo ulivyokuwa ukitekelezwa kwa uthabiti.
“Hakuna miraa inayoweza kuondoka JKIA ikiwa msafirishaji hajalipa. Mashirika ya ndege yana maagizo ya wazi ya kutekeleza ukusanyaji wa pesa hizo. Tulipolalamika 2022, tuliulizwa ikiwa pesa za wakulima zilihusika,” mfanyabiashara aliambia Taifa Leo.
Kurejeshwa kwa mauzo ya miraa nchini Somalia pia kuliashiria mwanzo wa udhibiti wa serikali wa biashara hiyo kupitia Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA).
Leave a Reply