Ndege nyingine yaanguka na kuua abiria 179 – Taifa Leo


WATU wasiopungua 179 waliangamia katika ajali ya ndege iliyotokea jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muan, kwa mujibu wa shirika la zima moto nchini humo.

Ndege hiyo ya kampuni ya Jeju Air iliyobeba abiria 175 na wahudumu sita wa ndege, ilikuwa inajaribu kutua mwendo wa saa tatu asubuhi katika uwanja huo eneo la kusini, wizara ya usafiri ilisema.

Ilikumbwa na hitilafu na kupoteza mwelekeo kabla ya kulipuka na kugonga ukuta.Mkuu wa idara ya zima moto, Lee Jung-hyun, alisema watu wawili ambao ni wahudumu wa ndege, waliokolewa huku akikadiria waliosalia, wote wanaoaminika kuwa raia wa Korea Kusini, wameaga dunia.Manusura, mwanamme na mwanamke ambao wote ni raia wa Thailand, waliokolewa kutoka sehemu ya nyuma ya ndege iliyosalia pekee na kupelekwa hospitalini kupata matibabu.

“Ni sehemu ya nyuma pekee iliyobaki, sehemu nyinginezo za ndege ni vigumu kutambulika,” alisema Lee.Ajali hiyo ya ndege ndiyo mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini Korea Kusini na mbaya zaidi inayohusisha shirika la ndege la Korea Kusini katika muda wa karibu miongo mitatu, kwa mujibu wa wizara.

Ndege hiyo aina ya Boeing 737-800 inayosheheni injini mbili ilionekana kwenye video iliyopeperushwa na vyombo vya habari ikiteleza kwenye mkondo wa kutua kabla ya kugonga ukuta na kulipuka.Picha nyingine zilionyesha ndege hiyo ikiwa imegubikwa na moshi na moto uliozimwa hatimaye saa saba adhuhuri.

Data kutoka wizara ya usafiri inaashiria kuwa ajali hiyo ndiyo mbaya zaidi inayohusisha shirika la ndege la Korea Kusini tangu 1997 wakati watu zaidi ya 200 waliangamia kwenye ajali ya ndege iliyofanyika Guam.

Ajali mbaya zaidi kuwahi kutokea Korea Kusini ilihusisha ndege ya shirika la Air China ambapo watu 129 waliuawa.Wataalam wanachunguza ndege aina ya nyuni na hali ya anga kama kiini cha ajali hiyo wakisema hitilafu ya kutua huenda ilisababishwa na nyuni.

Mnara wa kudhibiti safari za ndege ulitoa ilani ya ndege kugonga nyuni punde baada ya rubani kutangaza hali ya hatari, alisema waziri wa usafiri, pasipo kufafanua zaidi.Abiria mmoja aliripotiwa kumtumia jamaa yake ujumbe kumweleza nyuni amekwama kwenye ubawa wa ndege.“Niseme maneno yangu ya mwisho?” ulisema ujumbe wa abiria huyo.

Japo kiini cha ajali hiyo bado hakijabainishwa, mkasa huo umeangazia historia ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muan kuhusiana na visa sawia.Uwanja huo umeandikisha idadi kubwa zaidi ya matukio ya nyuni miongoni mwa viwanja 14 vya ndege Korea Kusini huku matukio 10 yakiripotiwa kati ya 2019 na Agosti mwaka huu, kulingana na data iliyowasilishwa bungeni na Taasisi ya Viwanja vya Ndege Korea.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*