HATUA ya Rais William Ruto kuungana na viongozi wa upinzani imeanza kubadili taswira ya kisiasa katika Kaunti ya Taita Taveta.
Wabunge katika kaunti hiyo waliochaguliwa kwa tikiti za vyama vya upinzani wameamua kumuunga mkono huku wakidai kuwa, hatua hiyo italeta maendeleo katika maeneo yao.
Hatua hii imezua gumzo katika ulingo wa kisiasa wa eneo hilo, huku Wabunge Peter Shake (Mwatate), John Bwire (Taveta), Danson Mwashako (Wundanyi), na Abdi Chome (Voi) wakitangaza hadharani kuwa watamuunga mkono Rais na kuwarai wenyeji ‘wasimsahau’ Dkt Ruto ifikapo uchaguzi wa 2027.
Hii ni licha ya kuwa, wakosoaji wanaonya kuwa mabadiliko haya yanaweza kudhoofisha jukumu la upinzani la kuikosoa serikali.
Mnamo Jumanne, wakati wa hafla ya kuwawezesha wanawake na vijana kujiendeleza kimaisha, Bw Bwire alisema kuwa, Mbunge Mwakilishi wa Kike, Bi Lydia Haika, alimshauri kuunga mkono serikali ili kuleta maendeleo katika eneo lake.
Bi Haika, aliyechaguliwa kwa tikiti ya chama cha UDA, ni miongoni mwa washirika wa karibu wa Rais Ruto katika eneo hilo.
“Dada yangu Haika amenionyesha upendo. Aliniambia kuwa mwaka wa 2027, wapigakura wangu watakumbuka maendeleo niliyoyafanya na sio maandamano dhidi ya serikali. Nilichukua ushauri huo na kuanza kutafuta marafiki kuona jinsi ya kubadilisha eneo langu. Rais ameahidi kufanya mengi katika eneo hili,” alisema.
Bw Bwire alitaja miradi ambayo tayari inaendelea katika eneo lake, akiihusisha na uhusiano wake mzuri na Rais.
Akizungumza katika hafla hiyo hiyo, Bi Haika aliwahimiza wakazi kuunga mkono serikali kwa ajili ya maendeleo.
“Huu ni wakati wetu kama kaunti. Tusisikilize kelele za nje. Wengine walinufaika na serikali zilizopita huku sisi hatujaona barabara za lami kama wengine, kwa hivyo huu ni wakati wetu. Tuikumbatie serikali,” alisema.
Aidha, aliihimiza jamii ya eneo hilo kuipa muda serikali kutekeleza miradi iliyoahidiwa.Akiongea katika eneo la Manga wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa Kiwanda cha Sh11 bilioni cha Devki cha kufua vyuma, ulioongozwa na Rais mapema mwezi huu, Bw Chome alimshukuru Bw Ruto kwa miradi ambayo serikali yake inatekeleza na kumwomba akamilishe baadhi ya miradi iliyokwama katika eneo hilo.
Hata hivyo, Seneta Jones Mwaruma ndiye kiongozi pekee katika kaunti hiyo ambaye hajajiunga na Rais Ruto kufikia sasa.
Aidha, aliomba lami kwa barabara mbili katika eneo lake na kumtaka Rais kutoa hati kwa chuo cha Ufundi cha Taita Taveta na kutoa basi kwa taasisi hiyo na Shule ya Sekondari ya David Kayanda.
Hata hivyo, Seneta Jones Mwaruma ndiye kiongozi pekee katika kaunti hiyo ambaye hajajiunga na Rais Ruto kufikia sasa.
Jumapili iliyopita, wakati Rais Ruto alipohudhuria ibada katika Kanisa la Soul Harvest mjini Taveta, Seneta Mwaruma pia alikuwa katika eneo hilo, akihudhuria ibada katika Kanisa la ACK St Dorcas Eldoro na baadaye hafla ya mahafali katika msikiti wa Masjid Ul Aqswa.
Seneta huyo vilevile alikosa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa Kiwanda cha kufua vyuma cha Devki, ulioongozwa na Rais na kuhudhuriwa na viongozi wote wa kaunti hiyo na maelfu ya wakazi mwanzoni mwa mwezi huu.
Bw Mwaruma amekuwa akikosoa serikali kuu kwa kutekeleza miradi michache ya maendeleo katika kaunti hiyo huku mingine ikikwama kwa sababu ya kutotengewa bajeti ya kutosha.
Leave a Reply