HATUA ya serikali kuvunjilia mbali Mamlaka ya kusimamia ukanda wa uchukuzi wa Bandari ya Lamu-Sudan Kusini-Ethiopia (LAPSSET), imeibua wasiwasi kuhusu hatima ya miradi mikubwa iliyotarajiwa kustawisha maendeleo katika Kaunti ya Lamu.
Miradi hiyo inayoanzia katika bandari ya Lamu hadi Kaskazini Mashariki mwa Kenya, sasa huenda ikatatizika baada ya baraza la mawaziri kuidhinisha kuvunjiliwa mbali kwa mamlaka ya kusimamia LAPSSET.
Katika tangazo hilo, mamlaka hiyo ilikuwa miongoni mwa mashirika mengine tisa ya serikali ambayo yaliorodheshwa kuvunjiliwa mbali.
Hata hivyo, serikali ilieleza kwenye taarifa hiyo kwamba shughuli za mashirika hayo zitatekelezwa na wizara husika.
“Baraza la mawaziri limependekeza kuvunjiliwa mbali kwa mashirika tisa ya kiserikali ambayo majukumu yao yamepitwa na muda,” serikali ilitangaza.
Mnamo Jumatano, duru katika mamlaka hiyo ziliambia Taifa Leo kuwa agizo lilitumwa kwa wafanyakazi kusimamisha mipango yote ya miradi iliyokuwa ikiendelea.
Kulingana na afisa katika mamlaka hiyo aliyeomba kutotajwa kwa kuhofia adhabu, mawasiliano kwao yalikuwa kwamba, wasubiri mwelekeo zaidi kutoka kwa wizara husika.
“Tumeambiwa tusubiri maagizo ya jinsi tutafanya kazi baada ya tangazo lililotolewa la kuvunja mamlaka katika kikao cha baraza la mawaziri Jumanne,” alisema.
Mamlaka ya LAPSSET ilizinduliwa mwaka wa 2012 wakati wa utawala wa Rais Mwai Kibaki.
Kwa sasa, miradi kadha kama ile ya kujenga barabara kuu ya Lamu-Garissa-Isiolo-Lodwar-Nakodok na Isiolo hadi Moyale ikiunganisha Ethiopia inaendelezwa.
Miradi mingine iliyotarajiwa kutekelezwa na mamlaka hiyo ambayo haijaanzishwa ni pamoja na reli ya kisasa (SGR) kutoka Lamu hadi Isiolo, Isiolo hadi Nakodok katika mpaka wa Kenya na Sudani Kusini.
Hatima ya kujenga bomba la mafuta kutoka Lamu hadi Isiolo hadi Nakodok pia sasa haijulikani.
Miradi mingine iliyokuwa imeorodheshwa kutekelezwa ni pamoja na uwanja wa ndege wa Lamu, Isiolo na Turkana.
Mnamo Agosti mwaka uliopita, miradi ya ukanda huo ilipigwa jeki baada ya mawaziri husika wa Kenya, Ethiopia na Sudani Kusini kutia sahihi mkataba wa kuwekeza kwa jumla ili kuharakisha miradi hiyo ambayo imejikokota kwa muda mrefu.
Leave a Reply