TULITAMATISHA sehemu ya pili ya makala kwa kueleza kuwa ni kosa kutumia kijalizo {ku} katika kitenzi cha silabi moja baada ya kujumuisha kiambishi cha nafsi katika kitenzi hicho hicho.
Kwa hivyo, mtangazaji wa runinga tuliyemtaja katika sehemu ya kwanza na ya pili ya makala angesema hivi: ‘Wakenya tunapaswa tuwe macho’ bali si ‘Wakenya tunapaswa tukuwe macho’.
Hata hivyo, msemaji wa kauli hii angekiepuka kiambishi cha nafsi kimakusudi katika kitenzi cha pili, kijalizo kingedumishwa ili kurahisisha matamshi. Hivi ndivyo kauli yenyewe ingeendelezwa: Wakenya tunapaswa kuwa macho.
Mazingira ya pili ya kisarufi ambamo kijalizo {ku} katika vitenzi vya silabi moja hutoweka ni wakati wa kuvikanusha vitenzi hivyo katika nyakati na hali mbalimbali isipokuwa wakati ujao. Tutarejelea kauli ya pili ilivyojitokeza katika makala fulani katika gazeti la Taifa Leo: ‘… hajakuwa akikubaliana kimahubiri na maombi ya EACC…’. Mwandishi wa kauli yenyewe alikuwa akirejelea utendakazi wa jaji fulani.
Nilivyotaja awali, neno ‘hajakuwa’ – ingawa usahihi wake tutakavyoona katika mistari michache ijayo ni ‘hajawa’ – katika uyakinishaji wake ni ‘amekuwa’.
Katika kukanusha hali ya {me} kijalizo cha kitenzi (-w-) hutoweka. Hali hiyo pia hudhihirika katika mazingira ya {li} na {hu} ambapo tunasema ‘hakuwa’ na ‘huwa’ bali si ‘hakukuwa’ na ‘hukuwa’ mtawalia.
Alhasili, matumizi mwafaka ya vitenzi vya silabi moja katika sentensi ni muhimu katika kufanikisha mawasiliano na kuepuka makosa ya sarufi.
Leave a Reply