HUU ni mwaka mpya na mambo mapya. Mathalan, Donald Trump ataapishwa kutumika kwa muhula wa pili kama rais wa Amerika, takriban majuma mawili yajayo, na mrejeo wake katika uga wa siasa za kimataifa utavuruga mambo si haba.
Kubwa zaidi kuhusu mrejeo huo ni nia ya Trump kuwachokoza na kuwahangaisha washirika wa muda mrefu wa Amerika, hasa ushirika wa kijeshi wa NATO. Kawaida ya fahali wanapopigana, nyasi huumia. Katika muktadha huu, Afrika ni nyasi kwa asilimia zote.
Trump ametishia pia kuanzisha vita vya kiuchumi dhidi ya mataifa tajiri kama Canada, Mexico na mengineyo ya Uropa.
Anatamani sana kufufua vita vya aina hiyo dhidi ya Uchina, na amesema atawafukuza wanajeshi wa Uchina wanaosimamia eneo la Panama zinakopitia meli.
Kumbuka wakati wa muhula wake wa kwanza – kati ya mwaka 2017 na 2021 – alipoanzisha vita hivyo dhidi ya Uchina viliathiri uchumi wa dunia kwa kiasi kikubwa, na mpaka sasa dunia ingali inapata madhara ya vita hivyo.
Tayari ametangaza kuwa ananuia kuitwaa Canada na kuifanya mojawapo ya majimbo ya Amerika, yaani Canada iwe jimbo la 51 la taifa hilo tajiri na lenye nguvu zaidi duniani.
Amesema atayapeleka majeshi ya Amerika kwenye Kisiwa cha Greenland, kwa maana ya kukitwaa na kukikalia, nao viongozi wa Kisiwa chenyewe wamesema hawakiuzi wala kukizawadia mtu!
Viongozi wa Canada nao wamesema hawana nia ya kuikabidhi nchi yao kwa Amerika, na hakuna ishara kwamba wabunge wa Amerika wataidhinisha hatua hiyo iwapo Trump atajaribu kuitekeleza.
Kimsingi, mataifa ya eneo la Amerika Kaskazini yana hofu kuu kwa kuwa haitabiriki Trump atayachokoza vipi, lakini yanajua ananuia kupanua mipaka ya Amerika ili kuyameza.
Hata ikiwa ni vitisho tu, hakuna nchi inayotamani kuwa na jirani mchokozi, hasa ikiwa ana dalili zote za kuwa na matatizo ya akili. Huhitaji kuwapima baadhi ya watu ndio ujue hawana akili razini. Wakipandwa na wa kwao ndipo utakapojua umeishi na mgonjwa siku zote.
Tatizo ni kwamba Trump ana wasaidizi ambao wana msimamo mkali, hasa kuhusu mipaka ya Amerika, na watapenda mno kuwa wawezeshaji wake katika uroho wa kutwaa nchi za watu, labda kwa kisingizio cha usalama wa kitaifa.
Historia inatuonyesha kwamba vita vya pili vya dunia vilianzishwa kwa njia hiyo ya kutamani nchi za watu na kuzitwaa ama kwa nguvu za kijeshi au kuwachochea wananchi dhidi ya tawala zao kabla ya kuingia huko na kutwaa hatamu za uongozi.
Kiongozi wa Ujerumani wa wakati huo, Adolf Hitler, alianzisha uroho huo na kuhimiza mno kuhusu umuhimu wa Wajerumani kuwa na nchi pana. Sijaona tofauti kati ya ya sera hiyo na mambo ambayo Trump anasema.
Trump mwenyewe amewahi kunukuliwa mara kadha akimsifia Hitler, jambo ambalo limewaudhi mno Wayahudi kwa kuwa ndio walioathiriwa zaidhi na unyama wa kichaa huyo.
Nina hakika kwamba mataifa mengi duniani yanahofia huenda Trump akawaingiza kwenye vita vya tatu vya dunia kimchezo, lakini hana uwezo wa kuwalazimisha kuvianzisha. Wanahitaji tu kutumia akili.
Nadhani ni kwa kutambua hilo ambapo viongozi wengi wa bara Uropa ambao wamekuwa wakiiunga mkono Ukraine katika vita vyake na Urusi wamelegeza misimamo yao na kuanza kuwasiliana na Rais Vladmir Putin wa urusi.
Trump angetamani hali ambapo Amerika itaingia vitani ikiwa upande mmoja na Urusi, ashirikiane na Putin kuyapiga mataifa na NATO na mengineyo ambayo hayajaonyesha wazi kwamba yanafungamana na Amerika katika masuala ya mahusiano ya kimataifa.
Kwa vyovyote vile, sera za utawala wa Trump zitaathiri Kenya na bara la Afrika kwa jumla, pamoja na mataifa mengine yanayoendelea.
Neno ‘msaada’ litasababisha Afrika ichukiwe na kudharauliwa na kiongozi huyo kwa kuwa ameapa dola za Amerika ni za Waamerika.
Ile tabia ya viongozi wetu kugeuka omba-omba wakifika Amerika itajibiwa kwa kero na dharau tele. Atawasikiliza wakipendekeza ushirikiano, si kusaidiwa.
Hata hivyo, ijapokuwa nimesema wawezeshaji wa Trump ni wengi, Amerika inajivunia mfumo wenye umadhubuti wa kiwango cha juu, tena hautegemei kiongozi wa nchi.
Kufoka ni haki yake, kutenda ni wajibu wa wataalamu wanaosimamia asasi za serikali.
Tutatoboa.
Leave a Reply