BAADA ya kutoonekana hadharani kwa muda wa miezi miwili, Gavana wa Nakuru Susan Kihika amefichua kuwa yuko likizo ya uzazi, na hivyo kumaliza uvumi kuhusu aliko.
Gavana Kihika hajaonekana hadharani tangu Novemba 18, mwaka jana, huku kukosekana kwake kukiibua mjadala katika vikao mbalimbali, ikiwemo mitandao ya kijamii.
Mnamo Ijumaa, Gavana Kihika alijibu suala hilo.
“Kufuatia simu nyingi ambazo nimepokea kuhusu kutokuwepo kwangu kama Gavana aliyechaguliwa wa Nakuru. Ninataka kuwahakikishia wakazi wa Nakuru kwamba niko mzima na kwa sasa niko likizo ya uzazi,” ilisema taarifa iliyotiwa saini na Dkt Peter Ketyenya, Mkuu wa Wafanyakazi Kaunti ya Nakuru.
“Huku nikiwashukuru wakazi wa Nakuru kwa kujali kwao, ninawahakikishia kwa moyo wote kwamba utoaji wa huduma katika kaunti yetu kuu unaendelea kama inavyotarajiwa chini ya uongozi mzuri wa timu inayoongozwa na Naibu Gavana David Kones,” ilisema taarifa hiyo.
Wakati huo huo, Gavana Kihika alisema kuwa atarejea kazini “wiki chache zijazo”, likizo yake itakapokamilika.
Bi Kihika hajaonekana hadharani kwa karibu miezi miwili huku watu wa familia na timu ya mawasiliano ikikosa kutoa maelezo.
Hakuna aliyekuwa tayari kujitokeza hadharani na maelezo kuhusu aliko gavana huyo. Bi Kihika alionekana hadharani mara ya mwisho mnamo Novemba 18, alipoongoza hafla ya kufuzu na kuwakabidhi vyeti vya ufundi wahitimu 4,146 kutoka vituo 33 vya Mafunzo ya Kiufundi katika Kaunti ya Nakuru.
Wakati huo alikuwa ameandamana na Naibu Gavana David Kones na maafisa wakuu wa kaunti. Baadaye alitoweka na hajawahi kuonekana tena hadharani.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply