WAKENYA hawatapata afueni ya mzigo wa ushuru unaowazonga hivi karibuni kwani serikali haijafaulu kukusanya kiwango lengwa cha mapato.
Waziri wa Fedha John Mbadi jana alisema kuwa serikali inaweza tu kupunguza viwango vya Ushuru wa Mshahara (PAYE) na Ushuru wa Thamani (VAT) endapo Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) itafaulu kukusanya kiwango lengwa cha mapato ya ushuru kwa angaa miezi sita mfululizo.
“Ukweli ni kwamba ni vizuri ikiwa ushuru utapunguzwa ili raia wapate afueni kiuchumi. Lakini wakati huu tunajikokota kulipa madeni yetu na hivyo hatua yoyote itakayopunguza kiwango cha mapato ya serikali haiweza kutelezwa wakati huu.
“Lakini endapo mageuzi ambayo tunatekeleza katika KRA yatazaa matunda na mamlaka hii iweze kutimiza kiwango lengwa cha mapato kwa miezi sita mfululizo, basi tunaweza kupunguza ushuru wa VAT na PAYE,” Bw Mbadi akasema jana asubuhi alipohojiwa katika kipindi cha Fixing The Nation katika runinga ya NTV.
Kauli ya Bw Mbadi inakinzana na ahadi aliyotoa wiki chache baada ya kuingia afisini Agosti mwaka jana kwamba serikali ingepunguza ushuru wa VAT kutoka asilimia 16 hadi asilimia 14 pamoja na PAYE (kwa wastani asilimia 30) na Ushuru wa Kampuni (asilimia 30 kwa mwaka).
“Nitawashangaza; katika mwaka ujao wa kifedha, tutapunguza viwango vya ushuru hasa ushuru wa VAT kutoka asilimia 16 hadi asilimia 14 ili kutoa afueni kwa Wakenya na kuchochea uchumi wa nchi,” Bw Mbadi akasema Septemba 9, 2024 alipozindua mchakato wa utayarishaji wa Bajeti ya Mwaka wa Kifedha wa 2025/2026. Katika kikao hicho, pia alidokeza kuwa PAYE na Ushuru wa Kampuni ungepunguzwa.
Hata hivyo, jana Bw Mbadi alisisitiza kuwa serikali haitaongeza au kuanzisha aina za ushuru aliotaja kama “kandamizi kwa Wakenya”.
Akizungumzia kuhusu mikakati ya kurejesha pesa katika mifuko ya wananchi, waziri huyo alisema tayari amepunguza makato ya bima ya SHA na Ushuru wa Nyumba.
“Baada ya kupitishwa kwa sheria ya Ushuru Desemba mwaka jana, kiwango cha ushuru wa Nyumba Nafuu na bima ya SHA kilipungua kwa asilimia 30.”
Aidha, Waziri alitetea sera za Rais William Ruto za kukusanya mapato akisema siyo kweli kwamba serikali inawabebesha raia ushuru mwingi kandamizi wanavyodai viongozi wa upinzani.
Bw Mbadi alisema kuanzishwa kwa ushuru wa nyumba na wa Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA) hakufai kufasiriwa kama njia ya kuwaongezea Wakenya ushuru.
Kulingana na waziri huyo, aina hizo za ada zinawafaidi pakubwa Wakenya.
“Siko upinzani. Niko ndani ya serikali. Mimi ni Waziri wa Fedha. Sipaswi kuongea mabaya kuhusu serikali, haiwezekani,” akasema Bw Mbadi huku akiahidi kwamba serikali itahakikisha hawatozwi ushuru kupita kiasi.
“Nimekadiria viwango vya ushuru na nikaona kwamba wizara yangu pia ina jukumu la kulinda mapato ya Wakenya,” Bw Mbadi akaongeza.
Februari 14 mwaka huu, waziri huyo wa Fedha anatarajiwa kuwasilisha bungeni Taarifa ya Kisera kuhusu Bajeti (BPS) inayoelezea jinsi serikali itakavyotumia pesa katika mwaka ujao wa kifedha wa 2025/26.
BPS pia itakadiria kiwango cha pesa ambazo serikali inapanga kukopa humu nchini na kimataifa ingawa kiwango cha ushuru unaokusanywa na serikali kilipungua katika miaka ya awali.
“Tumepunguza makadirio ya bajeti ya mwaka ujao wa kifedha kutoka Sh4.3 trilioni hadi Sh4.1 trilioni. Tunakadiria kukusanya Sh2.8 trilioni kutokana na ushuru mwaka huo. Kwa hivyo pengo la Sh1.3 trilioni litatokana na mikopo na washirika wa ufadhili,” akasema.
Viwango vya ushuru utakaotumiwa kufadhili bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2025/26 vitajumuishwa katika Mswada wa Fedha wa 2025. Hadi alipoteuliwa kuwa waziri wa Fedha mwaka jana, Bw Mbadi ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa ODM amekuwa mkosoaji mkuu wa mipango ya kiuchumi ya serikali ya Rais Ruto.
Kwa mfano, anajulikana kwa kupinga vikali wazo la kuongezwa kwa Ada ya Kukarabati Barabara (RML) kutokana na bei ya petroli na dizeli kutoka Sh18 hadi Sh25 kwa lita moja.
Kwa sasa Bw Mbadi anaitetea serikali hasa kuhusu Ushuru wa Nyumba wakati ambapo umma unalalamikia kuwa gharama ya maisha ingali juu kutokana na kupanda kwa ushuru.
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ni kati ya viongozi wa kisiasa ambao wameisuta serikali ya Rais Ruto kwa kuongeza ushuru kila mara.
Leave a Reply