Nimewasamehe walioniteka nyara na kunitesa, asema Billy baada ya kuachiliwa – Taifa Leo


MMOJA wa vijana walioachiliwa Jumatatu baada ya kutekwa nyara kwa siku 15 amesema amewasamehe waliomfanyia ukatili huo.

Billy Munyiri Mwangi, mwanachuo aliyetekwa nyara na wanaume wanne anasema kuwa amewasamehe waliohusika.Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kuachiliwa huru, Bw Mwangi alisisitiza kuwa hana chuki dhidi ya waliomteka nyara na kumtesa.

Katika mahojiano ya kipekee baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, Bw Mwangi alisema anamshukuru Mungu kwamba yungali hai.Pia aliwashukuru wazazi wake ambao waliendelea kupigania kuachiliwa kwake, majirani na wakazi waliojitokeza katika mitaa ya Embu wakitaka aachiliwe bila masharti.

“Niliteswa kiakili na sikumbuki mambo mengi, itanichukua muda kupona. Hata sasa najihisi kuchanganyikiwa kiakili, nimechanganyikiwa na sikumbuki kila kitu kilichonipata nikiwa mikononi mwa walioniteka nyara. Nimewasamehe wote walionichukua na kunifungia katika chumba chenye giza. Nimewaacha mikononi mwa Mungu” alisema Bw Mwangi akiwa nyumbani kwa wazazi wake Embu.

Bw Mwangi alikumbuka jinsi alivyoachwa Nyeri na akasafiri kwa matatu hadi nyumbani kwake Embu Jumatatu. “Nina furaha kwamba niliweza kurejea nyumbani hata baada ya kupitia kuzimu mikononi mwa watekaji nyara wangu,” alisema.

Alisema mateso hayo yalikuwa mabaya zaidi maishani mwake tangu azaliwe. “Sijawahi kuwa katika hali kama hiyo lakini sina kinyongo chochote dhidi ya watekaji nyara kwa sababu makosa ni ya binadamu,” alisema Bw Mwangi.

Regina Wairimu, mamake Mwangi alisema alifurahi sana mwanawe aliporejea nyumbani salama.

“Mtoto wetu alirudi nyumbani baada ya kuachiliwa, tunafurahi kuwa yu hai. Alikuwa akikohoa kidogo lakini tulimpeleka hospitali ambapo alitibiwa na kuruhusiwa kuja nyumbani. Tunawashukuru wote walioingilia kati na hata kutusaidia kuomba aachiliwe,”alisema.

Bi Wairimu alisema watoto hawafai kuchukuliwa kama wahalifu wanapokosea.”Watoto wanatakiwa kukabidhiwa kwa wazazi kwa ushauri nasaha ikiwa watakosea lakini sio kudhulumiwa,” alisema.

Naye Gerald Karicha alisema familia imewasamehe watekaji nyara. “Kilichotokea kimepita. Tuna mtoto wetu na ndivyo tulivyotaka. Aliachiliwa mahali fulani huko Nyeri na kwa neema ya Mungu alifanikiwa kurejea nyumbani,”alisema.

IMETAFSIRIWA NA WINNIE ONYANDO



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*