‘Ninafurahia joto la wadhifa wa kiongozi wa wengi bungeni’ – Taifa Leo


KIONGOZI wa wachache bungeni, Junet Mohamed mnamo Jumanne, Februari 11, 2025 aligeuza bunge kuwa uga wa ucheshi akielezea jinsi anavyohisi baada ya Mahakama kutoa maamuzi kuwa Azimio ndio mrengo wa wengi Bunge la Kitaifa.

Hii ni baada ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu wiki iliyopita kuamua kufuatia kesi iliyowasilishwa kortini, kuwa Azimio ndio muungano wenye wawakilishi wengi bungeni.

Azimio inajumuisha chama cha ODM, Jubilee, Wiper, Narc-Kenya, KANU, kati ya vyama vingine vya kisiasa nchini vilivyoungana 2022 kusimamisha mgombea wa urais.

Uamuzi wa Mahakama Kuu unaashiria kuwa muungano huo wa upinzani unapaswa kutwaa wadhifa wa spika, kiongozi wa wengi bungeni na pia kiranja wa wengi.

Kwenye kikao kujadili maamuzi ya mahakama, Bw Junet ambaye ni mbunge wa ODM, alisababisha wabunge kuangua kicheko akisema ameanza kuhisi joto la kuwa kiongozi wa wengi bungeni.

“Sijioni nikiacha wadhifa huu wakati wowote,” alisema mbunge huyo wa Suna Mashariki.

Bw Moses Wetangula ndiye Spika wa Bunge, mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wah naye akiwa kiongozi wa wengi na mwenzake wa Mugirango Kusini, Silvanus Osoro akishikilia nafasi ya kiranja wa wengi.

Junet na Millie Odhiambo – ambaye ni mbunge wa Suba Kaskazini na pia kiranja wa wachache, wanamezea mate wadhifa wa Ichung’wah na Osoro.

Bw Junet kwenye mdahalo bungeni kuhusu suala hilo, aliwataka walioathirika kuitikia maamuzi ya korti au kukata rufaa.

“Kuna maamuzi ya korti yaliyotolewa na jopo la majaji watatu, na walioathirika wanapaswa kuyaheshimu au wakate rufaa,” alielezea.

Azimio inaongozwa na kinara wa ODM, Raila Odinga, licha ya Waziri Mkuu huyo wa zamani kushirikiana na serikali ya Kenya Kwanza – mrengo wa Rais William Ruto.

Imekuwa mila na desturi viongozi wa wengi bungeni kuchaguliwa kutoka kwa mrengo wa rais aliye madarakani.

Mjadala huo ukionekana kuzua tumbojoto miongoni mwa wabunge wanaoegemea upande wa Rais Ruto, Junet Mohamed aliwataka kuheshimu uamuzi wa korti.

Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa Bw Odinga, alitumia mfano jinsi Azimio iliheshimu maamuzi ya Mahakama ya Upeo nchini katika kesi ambayo muungano huo iliwasilisha kupinga ushindi wa Rais Ruto 2022.

“Maamuzi ya korti ni muhimu sana. Baada ya uchaguzi, tulipinga ushindi wa rais katika Mahakama ya Juu zaidi nchini na uamuzi wa korti ulipotolewa tuliuheshimu,” Junet alisisitiza.

Mwaka uliopita, 2024, Rais Ruto na Bw Odinga walitangaza kuweka kando tofauti zao za kisiasa hatua iliyochangia kuundwa kwa serikali jumuishi – ambapo baadhi ya wandani wa Waziri Mkuu huyo wa zamani waliteuliwa kujiunga na Baraza la Mawaziri wa Dkt Ruto.

“Kuna huyu mnyama anayeitwa Serikali Jumuishi, tunataka kuipanua hata bungeni,” Bw Junet alisema.

Huku mjadala wa ni muungano upi unapaswa kushikilia nyadhifa za wengi bungeni ukionekana kubadili dira ya siasa za nchi, Bw Wetangula aliambia wabunge kuwa uamuzi wa korti haukuelezea anayepaswa kutwaa nafasi ya spika, kiongozi wa wengi bungeni na pia kiranja wa wengi.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*