Nitaungana na Karua, wengine kumshinda Ruto 2027 – Taifa Leo


KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka mnamo Jumamosi Februari 22 aliahidi kushirikiana na mwenzake wa Narc Kenya Martha Karua kumshinda Rais William Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Alifichua kuwa alikuwa akishauriana na vigogo wa kisiasa wanaopinga serikali ya Kenya Kwanza ili kuwakomboa Wakenya kutoka kwa kile alichotaja kuwa ‘minyororo ya ukandamizaji.’

‘Wiki ijayo, nitaungana na Martha Karua, ambaye atakuwa akibadilisha jina la chama chake. Tuko katika demokrasia ya vyama vingi vya siasa, na lazima tushikane mikono ili tunusuru nchi yetu isiharibike,’ alisema.

Bw Musyoka alisema tayari amekutana na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa na kueleza nia yake ya kutaka Bi Karua ajiunge nao.

‘Ni kweli nilikunywa chai na Rigathi na Wamalwa. Ni lazima tushirikiane kama timu kuhakikisha uongozi unabadilika kupitia kura,’ alisema.

Bw Musyoka alisema wanalenga kujenga upinzani mkubwa wenye uwezo wa kupinga Kenya Kwanza katika uchaguzi ujao.

“Tumeazimia kumpeleka Ruto Sugoi (nyumbani kwake kijijini) 2027. Wakenya wamechoshwa na uongozi mbaya ambao hauna uwazi,” akasema Bw Musyoka.

Aliitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ambayo itazinduliwa Mei, kudumisha uwazi katika uchaguzi wa 2027.

Aliapa kwamba upinzani hautaruhusu kuibiwa kwa kura.

Akizungumza katika Kanisa la Kianglikana la Rwang’ondu Kaunti ya Kirinyaga wakati wa harusi ya Samson Wanjohi na Josephine Wanjira, alisisitiza kuwa wizi wa kura hautavumiliwa tena.

‘Muungano wa Ruto haukushinda kura zilizopita. Uchaguzi hautavurugwa tena-haitafanyika,’ alisema.

Alisisitiza kuwa IEBC haifai kukubali kuhujumiwa na Serikali.

‘Tutakuwa macho. Tutahakikisha kuwa IEBC itaandaa uchaguzi wa kuaminika,’ alisema.

Wakati huo huo, Bw Musyoka aliitaka serikali kukoma kuingilia uhuru wa idara ya mahakama.

Alitaka mahakama ziruhusiwe kutekeleza wajibu wake bila vitisho.

“Serikali inataka mahakama itakayowapendelea iwapo kutatokea uchaguzi wenye utata, mahakama ikidhibitiwa na Serikali itakuwa mbaya sana,” alisema.

Bw Musyoka aliapa kuhakikisha kuwa idara ya mahakama inasalia kuwa huru.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*