Nitawaaibisha wote wanaonipinga – Ruto – Taifa Leo


RAIS William Ruto jana aliwahakikishia Wakenya kuwa ufanisi mkubwa kwenye nyanja mbalimbali za kiuchumi unakuja akisema ametumia miaka miwili ya utawala wake kuweka mikakati na msingi thabiti wa kuendeleza nchi.

Kiongozi wa nchi alikiri kuwa utawala wake umekuwa ukiyumbisha na changamoto ambazo hazijaisha ila matunda yameanza kuonekana na makubwa yako njiani kabla ya muhula wake wa kwanza kutamatika.

“Nina matumaini kuwa hali ya baadaye ya taifa letu ni nzuri na ajenda ya kubadilisha nchi hii itafanikiwa. Nimeweka msingi na mikakati, kazi imekuwa ikifanyika na Wakenya wametoa mchango wao,” akasema Rais Ruto.

Wanaotakia nchi mazuri

“Najihesabu miongoni mwa mamilioni ya Wakenya wanaotakia nchi yetu mazuri. Hakika tunasukumwa na ari ya kuwa na taifa bora na hilo liko njiani kwa sababu tumevumilia na mbele ni kuzuri,” akaongeza.

Rais Ruto alikuwa akiongea jana katika bustani ya Uhuru Gardens, Nairobi alipoongoza nchi kwa maadhimisho ya miaka 61 tangu Kenya ijinyakulie uhuru.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Rais wa Gambia Adama Barrow aliyekuwa mgeni wa heshima,. Viongozi wa ngazi mbalimbali wa utawala pia walikuwepo.

Akionekana kutilia manani vita ambavyo vimekuwa vikielekezewa serikali yake mitandoni kutokana na sera zake za kiuchumi hasa ushuru wa juu, Rais aliwahimiza Wakenya kuwa subira yao inaelekea kuvuta heri.

“Tangu mwanzo nia yetu ilikuwa kuweka msingi wa kushusha gharama ya maisha, kuongeza uzalishaji, kubuni nafasi za ajira, kuimarisha miundomsingi, kuwavutia wawekezaji kisha kutengeneza bidhaa, ujenzi wa viwanda na kuongeza bidhaa tunazouza nje ya nchi,” akasema.

Hata kabla ya mazuri haya ya ‘Canaan’ kuonekana, alijipigia debe kuwa wakati wa utawala wake wa miaka miwili, bei ya vyakula imepungua na kushusha gharama ya maisha.

Kenya inajitosheleza kwa chakula

Alisema kuwa Kenya sasa inajitosheleza kwa chakula ambapo katika maghala ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) kuna magunia milioni 95 ya kilo 50 za mahindi, milioni tisa ya maharagwe, milioni 10 ya ngano na milioni mbili ya mchele.

Rais alitaja hatua zilizopigwa katika sekta ya kilimo kuwa zilizotokana na serikali yake kutoa pembejeo za kilimo hasa mbolea ya bei nafuu kwa wakulima.

Utawala wa Dkt Ruto uliingia mamlakani kwa lengo la kuwainua wafanyabiashara wadogo wadogo na watu wenye mapato ya chini ndiposa ukaanzisha Hazina ya Hasla.

Nia ya kuanzisha hazina hii ilikuwa kuwaokoa vijana ambao walikuwa wakikimbilia mikopo yenye riba ya juu kisha kuorodheshwa vibaya na Mashirika ya Kufuatilia Mikopo (CRB) wanaposhindwa kuilipa.

Jana, Rais alisema hazina hiyo ambayo itaadhimisha mwaka wake wa pili imetoa mkopo wa Sh60 milioni na kwa wale ambao wamekuwa wakilipa mikopo yao bila kufeli, sasa kuna fursa ya kuchukua mingine.

Ajira kupitia mitandaoni na malipo kwa wasanii pia ilitengewa sehemu kubwa ya hotuba yake, akisema kwa sasa taasisi 74,000 za umma zimeunganishiwa intaneti huku maeneo mengine 25,000 yakiwa na Wi-Fi.

Biashara zina intaneti

Baada ya kutimiza hilo serikali sasa imeelekeza macho katika kuhakikisha kuwa nyumba milioni 8.5 na biashara zina intaneti kwa sababu ajira mitandaoni ni kati ya mbinu ya utawala wake kupunguza ukosefu wa ajira.

Kupitia mpango wa Ajira Jitume, kuna mkakati unaoendelea kutekelezwa wa kuhakikisha kuwa Wakenya milioni 20 wanapata mafunzo ya teknolojia ili wachangie katika shughuli za kiuchumi.

Alipigia upato teknolojia mpya ya AI na Blockchain akisema itasaidia katika uvumbuzi wa kiteknolojia na kurahisisha mageuzi ya kiuchumi.

Katika usanjari huo, alisema anaona fahari kuwa huduma 20,855 za serikali sasa zinatolewa kwa njia ya mtandaoni ndiposa si lazima Mkenya asafiri katika afisi kupokea huduma.

“Hii imehakikisha kuwa kuna uwazi na uwajibikaji wala Wakenya hawalazimiki kulipa hongo wanaposaka huduma za serikali,” akasema Rais.

Mfumo wa Bima ya Afya ya Kijamii (SHA) umekuwa ukilalamikiwa na Wakenya wengi ila serikali inaonekana kutorejea nyuma kwenye azma yake ya kuitekeleza.

Rais alisema Wakenya milioni 5.6 wamehamishwa kutoka bima ya zamani ya NHIF na ndani ya miezi miwili tangu bima hiyo ianzishwe, Wakenya milioni 11 wamesajiliwa.

Utekelezaji wa bima ya SHA

Bima hiyo mpya imekuwa ikilalamikiwa katika utekelezaji wake, Wakenya wanaosaka matibabu wakilazimika kutoa hela mifukoni mwao baada ya hospitali za umma na za kibinafsi kukataa kuwapa baadhi ya huduma.

Kiongozi wa taifa pia alisema ujenzi wa nyumba za gharama nafuu umetoa nafasi 200,000 za ajira kwa muda wa miaka miwili iliyopita.

Kupitia mpango huo nyumba 840,000 zitajengwa katika miaka minne ijayo ambapo nafasi za ajira milioni moja zinalengwa kubuniwa. Kwa sasa nyumba 124,000 zinaendelea kujengwa na nyingine 4,888 ziko tayari na Wakenya wako radhi kuzinunua kupitia mpango wa Boma Yangu.

Mbali na ufanisi mwingine alioutaja, Rais alionekana kuwachoka Wakenya wanaopinga kila mradi wa utawala wake, akisema atawavumilia kwa kuwa anaamini watazinduka wakiona matunda ya kazi yake.

“Kukosa kusimama na ukweli kunasawiri taifa letu vibaya. Hata tunapopinga, tuchapishe habari za ukweli mtandaoni badala ya kusambaratisha na kuharibu nchi yetu,” akasema.

Akikejeliwa na kuitwa muongo

Kauli yake inatokana na jinsi amekuwa akikejeliwa na kuitwa muongo baada ya kulemewa kutimiza miradi ya maendeleo aliyoahidi mnamo 2022.

Baada ya kupewa jina Zakayo, Wakenya wamempa jina Kasongo Yeye wakiendelea kumkejeli hasa baada ya wandani wake kuonwa kama waliojaa uongo kisha kugeuka wakali kwa Wakenya wanapouliza maswali kuhusu utendakazi na sera duni.

Rais alisema ataendelea kushirikiana na viongozi mbalimbali hata wale ambao hawakumuunga mkono mnamo 2022 kwa kuwa ajenda yake ni taifa moja ambalo litamwezesha kufanikisha ahadi ya kubadilisha nchi kimaendeleo.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*