IDARA ya Upelelezi wa Jinai (DCI) sasa inamtaka Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi kufika katika afisi zake kuandikisha taarifa kuhusu madai ya kutekwa nyara kwa mwanawe wa kiume Juni mwaka jana.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumapili, Januari 12, 2025 jioni, Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin alisema uchunguzi kuhusu kisa hicho umekuwa ukiendelea polepole kwa sababu mwanawe Muturi ndiye mtu wa pekee aliyeandikisha taarifa kuhusu kisa hicho.
Bw Amin alikuwa akijibu taarifa ya awali iliyotolewa na Bw Muturi kwa wanahabari jijini Nairobi ambapo alihoji kutojitolea kwa asasi za usalama, na za uchunguzi, katika kutanzua kitendawili kuhusu visa vya utekaji nyara na kutoweka kwa watu kwa njia ya kutatanisha.
“Kesi hiyo ambapo inadaiwa mwana wa kiume Waziri Justin Muturi alitekwa nyara ingali inashughulikiwa katika Afisi ya DCI, eneo la Kilimani, Nairobi. Kwa kuwa ni mwanawe pekee aliyejitokeza kuandikisha taarifa, tungependa kumwalika Waziri Muturi na mtu mwingine yeyote mwenye habari kuhusu kisa hicho aandikishe taarifa na DCI, Kilimani,” Bw Amin akasema kwenye taarifa iliyotiwa saini kwa niaba yake na John Marete.
Bw Amin alieleza kuwa uchunguzi wa DCI kuhusu kisa hicho uko katika viwango mbalimbali na faili itawasilishwa kwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) baada ya kukamilika.
“Tunaendelea kuomba usaidizi kutoka kwa wananchi wenye habari ambazo zinaweza kusaidia katika uchunguzi kwa waziwasilishe kwetu kwa siri. DCI inakariri kujitolea kwake kuhakikisha kuwa visa vyote vya uketaji nyara vinachunguzwa kikamilifu na wahusika wanachukuliwa hatua za kisheria,” akaeleza.
Mnamo Juni 23, 2024, mwanawe Muturi Leslie Muturi aliripotiwa kutoweka akishukiwa kutekwa nyara na watu waliodaiwa kuwa maafisa wa usalama katika mtaa wa kifahari wa Lavington, Nairobi.
Mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenje ndiye alifichua kuhusu kisa hicho.
“Leslie Muturi, mwana wa kiume wa Mwanasheria Mkuu (sasa Waziri wa Utumishi wa Umma) Justin Muturi ametekwa nyara na watu wanaooenaka kuwa maafisa wa usalama. Nilikuwa nikiendesha gari langu nyuma ya lake na nikashuhudia tukio hilo,” akasema akisimama kando ya gari la Leslie.
Hata hivyo, polisi, wakati huo, walikana kuwa na habari zozote kuhusu tukio hilo.
Ilisemekana kuwa Leslie, 4I, ambaye ni mfanyabiashara, alikuwa akijiburudisha katika klabu moja iliyoko kando ya barabara ya Dennis Prit, Nairobi, na alipoondoka ndipo akasimamishwa akatolewa nje na kuingizwa kwa gari jingine lililoondoka mara moja. Lengo la kutekwa nyara kwake halikujulikana.
Jumapili, Januari 12, 2025 akiwahutubia wanahabari katika mkahawa wa Serena, Nairobi, Waziri Muturi alielezea jinsi familia yake ilipitia mahangaiko baada ya mwanawe kutekwa nyara huku polisi ikidai kutokuwa na habari kuhusu tukio hilo.
Alisema alituma maombi kwa asasi mbalimbali za usalama lakini hakupata jibu.
“Sikuwa na uhakika kama mwanangu alikuwa hai au la, hali iliyotufanya kuhangaika na kuingiwa na majonzi kama familia,” akaeleza.
Bw Muturi alishangaa kuwa zaidi ya miezi sita baada ya tukio hilo na kuachiliwa kwa mwanawe, hakuna mshukiwa yeyote amefunguliwa mashtakiwa kuhusiana na kisa hicho.
“Aidha, hamna ambaye ametoa maelezo kuhusu sababu iliyochangia kutekwa nyara kwa mwanawe na kuzuiliwa kiasi cha kutoweza kuwasiliana na jamaa, marafiki na hata wakili wake,” Bw Muturi akasema.
Waziri huyo wa Utumishi wa Umma vile vile alionekana kuisuta serikali, anayoitumikia, kuhusiana na visa vya utekaji nyara wa watu, haswa vijana, wanaosawiriwa kuwa wakosoaji wa utawala huu wa Kenya Kwanza.
“Hamna shida ikiwa tutakosolewa kama serikalini; ukosoaji ndio sehemu ya sifa za utawala wa kidemokrasia unaoendelezwa katika taifa hili,” Bw Muturi akasema.
Kauli ya Muturi ilijiri siku chache baada ya kuachiliwa kwa vijana watano kati ya sita waliodaiwa kutekwa nyara kati ya Desemba 17 na Desemba 25, mwaka jana.
Wao ni Billy Mwangi, Ronny Kiplangat, Gideon Kibet, almaarufu Kibet Bull na Benard Kavuli.
Hata hivyo, Steve Mbisi aliyetekwa nyara eneo la Mlolongo, kaunti ya Machakos, Desemba 17, 2024 bado hajulikani aliko.
Ilidaiwa kuwa Wakenya hao wenye umri wa kati ya miaka 34 na 23, walitekwa nyara kwa kusambaza jumbe, picha na vibonzo vya kuikosoa sifa serikali na kuwadhalilisha viongozi wakuu katika utawala huu wa Rais William Ruto.
Bw Muturi ndiye waziri wa kwanza katika serikali kujitokeza kimasomaso kulaani visa hivyo vya ukiukaji haki za kibinadamu na kuelekeza kidole cha lawama kwa serikali.
Leave a Reply