Nyamazeni iwapo hamna maono, Omtatah ajibu wanaokosoa azma yake – Taifa Leo


SENETA wa Kaunti ya Busia Okiya Omtatah amesimama kidete na kuwapuuza wanaokosoa azma yake ya urais 2027 akiwataja kama wasio na ujasiri, maono, maadili na mawazo ya kubadilisha nchi.

Alipotangaza kuwa ameunda kamati ya kutathmini ufaafu wake kama mgombea urais katika uchaguzi mkuu ujao, baadhi ya wanasiasa walikosoa na kukejeli hatua yake baadhi wakisema hatoki jamii yenye ushawishi katika siasa za kitaifa na hana uwezo wa kifedha wa kufadhili kampeni za urais.

Wadadisi wa siasa wanasema waliokosoa azma ya Bw Omtatah ni washirika wa karibu na vigogo wa kisiasa ambao wamekuwa wakinufaika na serikali ya sasa na zilizotangulia na lengo lao ni kudumisha na kuendeleza mtindo wa sasa wa siasa ili kulinda maslahi yao.

mawazo mapya

Akimjibu mwanasiasa Fredrick Okango mnamo Jumamosi, Novemba 23, 2024, Omtatah alisema kwamba ingawa siasa mara nyingi zimeonekana kutegemea idadi ya kura za jamii anayotoka mgombeaji, ana imani kuwa ni kutoa mawazo mapya na kuwaunganisha Wakenya katika maadili ya pamoja ambako ni muhimu zaidi.

Kulingana na Omtatah, mabadiliko ya kweli huanza kwa kupinga hali iliyopo, ambayo anasema amejitolea kikamilifu.

Hata kabla ya kuwa seneta, Omtatah alikuwa mtetezi mkuu wa haki za raia akiwasilisha kesi dhidi ya serikali alipohisi iliweka sera na sheria za kukandamiza umma.

Mwanasiasa huyo ambaye ni mwanaharakati wa miaka mingi, amewataka wakosoaji wake kuacha kumkosoa na badala yake waungane naye kuelekea nchi katika enzi ambazo uongozi utaamuliwa na maono badala ya idadi ya watu wa kabila analotoka mwaniaji.

“Ndoto ni muhimu sana, lakini pia ujasiri. Ingawa siasa mara nyingi zimeonekana kutegemea idadi, ninaamini pia inahusu kutoa mawazo mapya na kuunganisha Wakenya kuhusu maadili ya pamoja. Mabadiliko ya kweli huanza na changamoto na nimejitolea kwa safari hii. Wacha tufanye kazi kuelekea siku zijazo ambapo uongozi unafafanuliwa kwa maono, sio tu idadi na makabila,” Omtatah alisema.

Okango alikuwa amepuuzilia mbali azma ya urais ya Omtatah kwa kile alichokitaja kama ukosefu wa ngome thabiti au ushawishi kitaifa.

ngome imara

Seneta wa Nandi Samson Cherargei pia alipuuzilia mbali azma ya Omtatah ya urais 2027 kwa msingi kwamba alihitaji ngome imara ya wapiga kura na angalau Sh7 bilioni  kufanikisha  kampeni ya urais.

Cheragei pia alisema kuwa Omtatah anahitaji mtandao wa mashinani ilhali hata hana wa kijamii.

“Kwa kaka yangu na seneta mwenzangu @OkiyaOmtatah huku nikikutakia heri katika azma yako ya urais, nina mambo machache unayohitaji kufahamu kama vile kuendesha kampeni ya urais yenye mafanikio unahitaji angalau Sh 7 bilioni; mtandao mashinani na pia kushindana na Ruto ni vigumu iwapo alimshinda mgombeaji wa serikali Raila odinga katika uchaguzi Mkuu wa 2022,” Cherargei alisema.

Katika uchaguzi mkuu wa 2022, Rais Ruto alishindana na Raila Odinga aliyekuwa akiungwa mkono na rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta. Hii ilimfanya Bw Odinga kubatizwa mgombeaji wa serikali.

uongozi hauhusu utajiri

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli pia alipuuza azma ya Omtatah  kutwaa urais 2027 akisema ni mtu maskini naye seneta huyo akamwambia uongozi hauhusu utajiri.

“Uongozi unahusu maono, uadilifu, na nia ya kuhudumu. Wakenya wa kawaida ndio uti wa mgongo wa vuguvugu lolote la kweli la mabadiliko. Tutathibitisha kuwa kampeni inayoongozwa na watu inaweza kutia matumaini na kutoa mustakabali mwema kwa maisha ya wote,” Omtatah alimwambia Atwoli ambaye huwa anajipendekeza kwa kila serikali inayoingia mamlakani tangu enzi za Kanu.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*