Nyamita aapa kuendelea kuwa mshirika wa Rais Ruto eneo la Nyanza – Taifa Leo


MBUNGE wa Uriri Mark Nyamita ameapa kuendelea kufanya kazi na Rais William Ruto licha ya kwamba baadhi ya wanasiasa wa ODM bado wanashikilia kuwa chama hicho hakijajiunga na serikali.

Mbunge huyo alisema anashirikiana na kiongozi wa taifa kwa manufaa ya wakazi wa eneobunge lake na kaunti ya Migori kwa ujumla.

Bw Nyamita aliyechaguliwa kwa tikiti ya ODM alisema amekuwa akishambuliwa kwa kuamua kushirikiana na Rais Ruto ambaye ndiye kiongozi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Alisisitiza kuwa ataendelea kufanya mazungumzo na kiongozi wa taifa ili afanikishe utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo eneobunge la Uriri.

Mwaka jana, 2024, Bw Nyamita ni miongoni mwa wabunge watano wa ODM waliotajwa kama waasi kwa kumtembelea Rais Ruto katika Ikulu ya Nairobi.

Wengine walikuwa Gideon Ochanda (Bondo), Elisha Odhiambo (Gem), Phelix Odiwuor (Langata), Tom Ojienda (Seneta wa Kisumu), Caroli Omondi (Suba Kusini) na Paul Abuor (Rongo).

Wiki jana, Bw Nyamita aliwakaribisha maafisa wakuu wa kampuni ya kuzalisha umeme nchini KenGen waliozuru eneobunge lake kusambaza hatimiliki kwa familia zinazopakana na kiwanda cha kuzalisha stima cha Gogo.

KenGen inapanga kupanua mradi huo ili uweze kuzalisha megawati 8.6 ya stima kutoka megawati mbili inayozalisha sasa.

Bw Nyamita alisema hiyo ni miongoni mwa miradi ambayo Rais Ruto aliahidi kutekelezea eneo hilo.

Kiongozi wa taifa alitoa ahadi hiyo Agosti 4, mwaka huu, alipokutana na wabunge kutoka eneo la Luo Nyanza katika Ikulu Ndogo ya Kisumu.

 

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*