SENETA wa Kisii Richard Onyonka ameeleza kuwa jamii ya Abagusii itawasilisha aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i kuwania urais katika uchaguzi wa 2027.
Seneta huyo pia ameongeza kuwa jamii yake itaanzisha chama kipya itakachotumia kujinadi katika ulingo wa siasa za kitaifa akieleza kuwa wamekuwa wakitelekezwa katika teuzi za nyadhfa serikalini kwa kukosa chama.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, mbunge huyo wa zamani wa Kitutu Chache Kusini alisema katiba ya Kenya ya mwaka 2010 iliwakomboa kutoka vitendo visivyo vya kidemokrasia na kuwapa nafasi ya kufanya maamuzi huru ya kisiasa ambayo ni ya haki, uwazi na ukweli.
Kulingana na seneta Onyonka, baada ya viongozi wa jamii ya Abagusii kuangazia kwa kina matukio ya kisiasa yanavyoendelea nchini, waliafikiana kuwa na chama chao ili iwe rahisi kwao kutetea maslahi ya watu wao.
“Baada ya mashauriano na thathmini pana kuhusu siasa za Kenya, tumeamua kuwa tutabuni chama chetu kama jamii ili kulinda na kutetea maslahi yetu,” Seneta Onyonka.
Kiongozi huyo pia alimpongeza mwekahazina wa chama cha ODM Timothy Bosire kwa kukataa uteuzi wa kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usafiri na Usalama Nchini (NTSA).
Bw Onyonka alimsifu mbunge huyo wa zamani wa Kitutu Masaba kwa kukataa mnofu huo aliorushiwa na rais William Ruto, akimtaja kama Mkenya mzalendo ambaye hataki kujipaka tope katika serikali ya Kenya Kwanza aliyosema imefeli kuwatimizia Wakenya ahadi ilizowapa wakati wa kampeni.
“Tunamheshimu na kumuunga mkono Bw Bosire kwa kukataa kuuchukua mnofu huo ambao alirushiwa na serikali ambayo sera zake ni dhalimu na zisizofanya kazi,” Seneta Onyonka alisema.
Leave a Reply