SENETA wa Busia Okiya Omtatah alikamatwa Jumatatu wakati wa maandamano ya kulalamikia utekaji nyara wa wakosoaji wa utawala wa Rais William Ruto yaliyokumba baadhi ya maeneo ya Kenya.
Polisi walikuwa na wakati mgumu kumkamata seneta huyo na wenzake kadhaa waliokuwa wamejifunga kwa mnyororo kwenye barabara ya Aga Khan, Nairobi kwa saa kadhaa.
Bw Omtatah alijiunga na waandamanaji dakika chache baada ya kuwasilisha kesi katika mahakama ya Kibera alitaka Inspekta Jenerali wa polisi alazimishwe kutoa vijana kumi waliotekwa nyara Desemba kwa kukosoa serikali.
Watu kadhaa walijeruhiwa polisi walipowafyatulia waandamanaji vitoa machozi kuwatawanya huku Bw Omtatah na wenzake waliojifunga kwa mnyororo wakikaa ngumu.
Baadaye alasiri, polisi walifanikiwa kuwafungua na kuwasukuma ndani ya magari ya polisi kabla ya kuwapeleka vituo vya polisi jijini.
Waandamanaji walivamia kituo cha polisi cha Central wakitaka waliokamatwa waachiliwe ambako walitimuliwa kwa kurushiwa vitoa machozi.
Kabla ya polisi kutawanya waandamanaji ambao walikuwa wachache kuliko maandamano ya Juni- Julai 2024, jiji lilikuwa tulivu kiasi asubuhi.
Hata hivyo, walipotawanya waandamanaji waliokuwa watulivu, biashara zilizokuwa zimefunguliwa zilifungwa haraka kwa kuhofia kuporwa.
Japo waandamanaji hao walishikilia kuwa hawakuwa na silaha na walidumisha amani, polisi waliwataka warudi nyumbani wakisema hawakuwa na kibali kuandamana.
Chini ya sheria za Kenya, waandalizi wanatakiwa tu kuwaarifu polisi kuhusu maandamano.
Waandamanaji hao walikuwa na mabango ya baadhi ya waathiriwa wa hivi punde wa utekaji nyara yakiwemo ya Gideon Kibet, Ronny Kiplagat, Steve Kavingo Mbisi, Billy Mwangi, Peter Muteti, Bernard Kavuli na Kelvin Muthoni.
Kizaazaa sawia kilishuhudiwa katika mji wa Embu, takriban kilomita 130 kutoka Nairobi, ambapo ghasia zilizuka huku polisi wakipambana kuwazuia waandamanaji.
Mjini Mombasa, polisi waliwatawanya vijana waliokuwa wamekusanyika kwa maandamano katika bustani ya Uhuru Gardens, huku kamanda wa kaunti hiyo Peter Kimani akitangaza kuwa maandamano hayo yalikuwa haramu.
Kimani alidai kuwa hakuna utekaji nyara Mombasa na akapendekeza wanaotaka kuandamana wafanye hivyo Nairobi.
“Kuna utekaji nyara Mombasa? Halafu mbona mnaandamana hapa Mombasa? Mnapaswa kwenda kuandamana Nairobi. Nionyesheni kibali,” alisema.
Licha ya waandalizi hao kusema kuwa bustani ya Uhuru Gardens ni eneo la umma ambapo kila mtu alikuwa na haki ya kukusanyika, kamanda huyo aliwaamuru maafisa wake ambao walikuwa wamewazidi waandamanaji kuwatimua vijana nje ya bustani hiyo.
Waandamanaji, ambao walikuwa wamekusanyika saa mbili na nusu asubuhi, walipanga kufanya maandamano katika Pembe za Ndovu kwenye barabara ya Moi, eneo la kawaida la maandamano Mombasa.
Huko Kitengela, kitovu cha maandamano dhidi ya serikali yaliyoongozwa na vijana mnamo Juni katika Kaunti ya Kajiado, polisi waliweka kizuizi kwenye Barabara ya Namanga huku wakidhibiti watu kuingia katika mji huo.
Helikopta ya polisi ilionekana ikizungukazunguka hewani, ikifuatilia hali katika mji huo huku maafisa wakifanya kazi kuepuka uwezekano wa “vurugu kutoka nje”.
Ukaguzi uliofanywa na Taifa Leo Jumatatu asubuhi ulifichua kikosi cha maafisa wa polisi waliokuwa wamejihami vikali katika Kituo cha Polisi cha Kitengela wakiwa tayari kutumwa kukabiliana na hali yoyote.
Maafisa wa polisi waliokuwa wamejihami vikali waliosimamia kizuizi cha barabarani, mita chache kutoka Kituo cha Polisi cha Kitengela na katika mpaka wa kaunti ya Kajiado-Machakos, walikagua magari yote yaliyoingia mjini.
“Tuna maagizo ya wazi kutoka kwa wakuu wetu kutoruhusu watu wa nje kufanya fujo mjini kwa jina la maandamano ya kupinga utekaji nyara. Matukio kama haya yalishuhudiwa hapo awali,” afisa ambaye alizungumza na Taifa Leo kwa sharti asitajwe jina kwa sababu hana mamlaka ya kuongea na wanahabari alisema.
Wengi wa wenyeji waliozungumza na Taifa Leo walilaani utekaji nyara unaoendelea wa wakosoaji wa serikali, wakisema ni ukiukaji wa Katiba.
“Kuwateka nyara vijana wanaoikosoa serikali ni udikteta wa siku hizi ambao utazidisha uhusiano ambao tayari ulikuwa baridi kati ya utawala wa sasa na Wakenya,” Joseph Kamanu aliambia Taifa Leo.
Ingawa shughuli za biashara na uchukuzi zilikuwa kawaida, kulikuwa na watu wachache katika mji kwani wakazi wengi walimua kubaki nyumbani.
RIPOTI ZA NDUBI MOTURI, STEVE OTIENO, RICHARD MUNGUTI, GEORGE MUNENE, WACHIRA MWANGI NA FRIDAH OKACHI
Leave a Reply