SIJUI kama umewahi kuiskia kauli hii, ‘pesa haipendi kelele’.
Kwa bahati nzuri nimebahatika kutangamana na watu wenye pesa zao na nitakuambia hili, wengi sio watu wa kupenda kujishaua. Wanapenda kuendesha maisha na shughuli zao kimya kimya.
Kwenye Instagram ndio wale utakuwa akaunti zao zina followers 200 na kapicha kamoja ambako sio wao. Wanathamini sana usiri, na ukimya.
Hawa watu bwana huwa ndio wanaishi maisha matamu kweli kweli. Ila kama tujuavyo hamna masika yasiyokuwa na mbu, bado kuna watu wenye pesa ambao mashauo na kiburi ni pro-max.
Wanaturingishia mitandaoni maisha yao ya kifahari. Wengine ni watu waliostahili kulinda umri na heshima zao, lakini kiburi cha pesa kinawafanya kujisahau.
Mfano mzuri na Simon Kabu na mkewe Sarah. Hawa bwana ni watu wawili walioanza kujitafuta wakiwa hawana chochote. Wakaja wakajaliwa pesa na biashara kubwa. Wakapata umaarufu mitandaoni na hapo ndio wakaanza kuharibu.
Nakumbuka mapenzi yao yakiwa yameshamiri miaka ya nyuma huku pesa zikiwa zimeanza kuingia, walituhangaisha sana na kuturingishia maisha yao ya kifahari mitandaoni wakinunuliana ma Range Rover kama zawadi wakitupostia tuone jinsi mapenzi yao yalivyoshamiri na maisha yanawaendea poa.
Sasa bwana hawa matajiri wa Bonfire Adventures kwa sasa wanazo pesa zao ila raha ndio hawana. Ile kasumba yao ya kuishi wakiposti wanavyopendana imekuja kuwatokea puani.
Baada ya penzi lao kuingia mdudu walijaribu kukaa kimya na kwa sababu walizoea kututangazia ya kwako, mabloga wakaanza kuibuka na umbea kuwa penzi lao limeoza.
Madai ya kuchepukiana yakaibuka. Na kwa kuhofia kuharibu biashara yao, ikawalazimu wapenzi waanze kuanikana mitandaoni kila mmoja akijaribu kumlaumu mwenzie. Ikafikia wakati wakamwingiza mpaka kijakazi wao kwenye drama zao.
Sasa huyo kijakazi amewapeleka mahakamani na kuwashtaki kwa kumdhalilisha, kumtumia kama kisingizo kwenye skendo zao, na pia kumtumia kama chambo cha kiki mitandaoni kwa faida yao na biashara yao.
Kwenye kesi hiyo, amefichua mengi ya siri na sasa anadai fidia ya Sh21 milioni. Hapa nilipo nawaza, baada ya taarifa hizo kubebwa na gazeti la kitaifa la Daily Nation, hii inaiwacha wapi sura ya biashara yao lakini hata zaidi ni picha gani imewatengenezea.
Laiti wasingelikuwa wambea, na wakose muwasho wa kutaka kuturingishia maisha na fedha zao, pengine leo haya tusingeyafahamu. Sasa wanaangaziwa maana sio tu watu maarufu lakini pia ni matajiri.
Wote wawili ni watu wenye midomo chiriku, langu ni kusubiri kuona kama kesi hii itawatuliza midomo maana imewachomea.
Leave a Reply