
SHULE za sekondari katika maeneo yanayokuzwa muguka Kaunti ya Embu, zinakabiliwa na tishio la kufungwa watoto wakiacha shule kufanya kazi ya kuvuna zao hilo.
Shule ya Sekondari ya Gikiiro inayozingirwa na mashamba makubwa ya muguka Mbeere Kusini, Kaunti ya Embu, ilinusurika kufungwa watoto wakizamia biashara ya kuvuna muguka.
Hii ni kwa sababu biashara ya muguka imeshamiri katika eneo hilo jambo ambalo linavutia watoto na kuwafanya wasahau kuenda shule.
Kufikia mapema mwaka wa 2022, shule hiyo ilikuwa imesalia na wanafunzi 25 na kuichochea jamii na washikadau wengine kuchukua hatua ili wanafunzi warudi shuleni.
Hatua iliyochukuliwa na wakazi wa eneo hilo ilifanya idadi ya wanafunzi kupanda kutoka 25 hadi 100.
Kulingana na Bw David Muchoki, 20, ambaye aliacha shule katika darasa la saba, watoto wengi wanasukumwa katika ajira ya kuvuna muguka kutokana na ukosefu wa karo.
“Nilianza kuvuna muguka nikiwa na miaka 16 na ninaweza kujaza beseni tano na kupata hadi Sh500 kila asubuhi. Ningependa sana kufanya kozi ya kiufundi ila siwezi kwa sababu sina elimu inayohitajika,” Muchoki alisema.
Uchunguzi katika Shule ya Msingi ya Gatumbiri karibu na soko la Kiritiri unaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi imepungua kutoka 250 hadi 125 muhula huu.
Lakini usimamizi wa shule hiyo unadai kuwa kupungua kwa idadi hiyo kumetokana na kuondolewa kwa mpango wa lishe shuleni ambao watoto kutoka familia za mapato ya chini walitegemea.
Kulingana na chifu msaidizi wa Kianjiru, Bi Wanjiru Njiru, baadhi ya watoto hao wanaingizwa kwenye biashara ya muguka kutokana na umaskini.
“Katika eneo langu, niliweza kurudisha watoto sita ambao walikuwa wameacha shule ili kujitosa katika biashara ya muguka. Tumegundua mtindo ambapo wavulana wengi huacha shule wakiwa darasa la saba,” Bi Njiru alisema.
Mchungaji Cecily Nyaga, ambaye amekuwa akiendesha kampeni dhidi ya ajira ya watoto Mbeere Kusini, anasema watoto wengi pia huamka mapema kuvuna muguka kabla ya kwenda shule.
“Kwa sababu ya uchovu wa kazi ya asubuhi na mapema, hawawezi kukaa muda huo wote shuleni kusoma. Baada ya muda, wanakuwa watoro na kujikita katika biashara ya kuvuna muguka ili kupata pesa. Hii ndiyo sababu shule nyingi zina idadi kubwa ya wasichana ikilinganishwa na wavulana,” Bi Nyaga anasema.
Katika jitihada za kutatua tatizo hilo, mwenyekiti wa Ushirika wa Biashara wa Membe, Bw Peter Njeru, anasema wanatekeleza sheria ili kuhakikisha hakuna mtoto anayeshiriki katika biashara kama hiyo.
“Wakati pekee tunaruhusu watoto mashambani ni wakati wa likizo wakati wanasaidia wazazi wao. Tutahakikisha watoto wote wako shuleni,” Bw Njeru alisema.
Imetafsiriwa na Winnie Onyando
Leave a Reply