Pigo kwa Kabogo kesi ambayo mjomba anamdai fidia ya Sh387 milioni ikifufuliwa – Taifa Leo


KESI ya umiliki wa ardhi kati ya Waziri William Kabogo na mjombake Kimani Kabogo imerejeshwa katika Mahakama Kuu kusikilizwa na kuamuliwa.

Hii ni baada ya Mahakama ya Rufaa jijini Nairobi kufuta uamuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu Lucy Gacheru aliyetupilia mbali kesi hiyo.

Chanzo cha mzozo huo ambao umedumu tangu 2017, ni madai ya ulaghai na kuyeyusha uaminifu kwa upande wa Bw Kabogo, ambao Bw Kimani alisema aligundua mnamo 2006.

Aliwasilisha kesi 2017 akitaka Sh387 milioni kama fidia kutoka kwa Bw Kabogo.

Katika hukumu iliyotolewa na Majaji Abidah Ali-Aroni, Aggrey Muchelule na George Odunga, Mahakama ya Rufaa iliagiza mzozo huo usikizwe na kuamuliwa na mwingine lakini si Jaji Gacheru.

“Baada ya kuzingatia pingamizi iliyotolewa na Bw Kabogo katika Mahakama Kuu ambayo iliunda msingi wa uamuzi wa Jaji, tunaona kwamba, pingamizi ya awali haikuzingatiwa ipasavyo na haikupaswa kudumishwa. Kabla ya kufikia matokeo hayo, kulikuwa na suala la msingi la kuwepo kwa uaminifu ambalo lilipaswa kubainishwa,” walisema majaji

Ikiamua kuhusu rufaa iliyowasilishwa na Bw Kimani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, mahakama hiyo ilisema mahakama  ilitenda makosa ilipotupa kesi hiyo kwa msingi kwamba madai ya Bw Kimani yalizimwa kwa kuwa yaliwasilishwa nje ya muda uliowekwa wa miaka mitatu.

Mzozo huo unahusisha sehemu tatu za ardhi, ambazo Bw Kimani anadai Bw Kabogo alipata kwa njia ya ulaghai.

Kulingana na Bw Kimani, alikuwa mmiliki wa ardhi iliyosajiliwa kama LR.No.12825/27, LR.No.12825/33 na 12825/34  Machi 1998 alipotumia hatimiliki hizo kukopa Sh15 milioni kutoka benki ya NIC na ICDC.

Wakati fulani mnamo Septemba 2000 baada ya kushindwa kulipa mikopo hiyo kwa sababu ya viwango vya juu vya riba, aliomba msaada wa mpwa wake Bw Kabogo, ambaye alilipa mkopo katika Benki ya NIC kuzuia kuuzwa kwa  LR.No.12825/27 na 12825/34 kupitia mnada wa hadhara.

Karatasi za mahakama zinaonyesha kuwa maelewano yalikuwa kwa Bw Kabogo kushikilia mali  kwa dhamana kwa niaba ya  Bw Kimani hadi wakati ambapo ardhi hiyo ingeuzwa kwa thamani ya soko au kuendelezwa na mapato yagawanywe kwa usawa kati ya wawili hao.

Pia alikuwa ameomba usaidizi wa Bw Kabogo katika mwaka wa 2003 ili kuokoa Plot LR.No.12825/33, iliyokuwa ikikaribia kupigwa mnada na ICDC, ili kurejesha mkopo wa Sh5 milioni.

Kulingana na Bw Kimani, mnamo 2006 alipotaka kujua hali ya mali yake kutoka kwa Bw Kabogo ili waweke makubaliano ya mdomo kati yao kwa maandishi, Bw Kabogo alimkwepa.

Aidha alisema kwamba baadaye Bw Kabogo alimfurusha Bw Kimani kutoka kwa ardhi yake na kubomoa nyumba zake, kiwanda cha kahawa na nyumba za wafanyikazi na kumwacha bila makao na maskini.

Bw Kimani alidai kuwa tabia ya Bw Kabogo ilikuwa sawa na ulaghai na kuyeyusha uaminifu na ilimfanya kupata hasara na uharibifu wa Sh387,875,000.

Kwenye utetezi wake katika Mahakama Kuu, Bw Kabogo  alikanusha madai  dhidi yake.  Hasa alikanusha kwamba kuwepo kwa makubaliano ya kushikilia mali kwa dhamana kati yake Bw Kimani ilivyodaiwa.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*