MMOJA kati ya waumini 25 wa Kanisa Katoliki la Malongo Kaunti Ndogo ya Suba ya Kati walioenda kuuchukua mwili wa mmoja wao ameaga dunia baada ya gari lao kupata ajali.
Baadhi ya waumini wa kanisa hilo walikuwa wamefunga safari kutoka kijiji kilicho karibu na kanisa hilo kwenda katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Suba iliyoko Sindo kuchukua mwili wa Rose Odhiambo.
Kulingana na walioshuhudia kisa hicho, gari hilo lilipoteza mwelekeo na kubingirika. Raphael Obondo, 68 alikuwa mmoja kati ya wale waliopata majeraha na kulazwa katika hospitali ya Kaunti ndogo ya Suba mjini Sindo ila akaaga dunia akipokea matibabu.
Kulingana na Bw Nicholas Ochieng’, aliyenusurika, gari hilo lilipoteza mwelekeo lilipokuwa likipiga kona.
“Tulikuwa tumepita tu kanisa letu wakati gari lilipoteza mwelekeo ghafla. Kila mtu aliyekuwa nyuma alirushwa nje,” alisema.
Kulingana na ripoti ya polisi, watu 16 walipata majeraha mabaya huku wengine tisa wakipata majeraha madogo.
Waliopata majeraha mabaya walilazwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Suba huku wenzao waliopata majeraha madogo wakitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Bw Ochieng alisema ajali hiyo ilitokea kwa sababu gari hilo lilibeba abiria wengi.
Chifu Msaidizi wa Kitongoji cha Malongo, Bonface Sakwenda alisema baadhi ya watu waliojeruhiwa walipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay.
“Wale ambao wako katika hali mbaya walipewa rufaa kupata matibabu zaidi ili kuokoa maisha yao,” akasema Bw Sakwenda.
Leave a Reply