Presha Atwoli, Ichungwa, Sudi na wengine waitwe kortini – Taifa Leo


CHAMA cha wanasheria kutoka Mlima Kenya kinataka viongozi wanane miongoni mwao Francis Atwoli, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah na Spika wa Seneti Amason Kingi kuitwa mahakamani kufuatia matamshi yao ya kumhusisha aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua na utekaji nyara.

Chama hicho kinasema itakuwa haki wito kutolewa kuwalazimisha watu hao kufika mbele ya mahakama kuhojiwa.

Chama hicho pia kinataka kujiunga na kesi iliyowasilishwa Desemba na Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK), ambacho kinataka serikali ilazimishwe kuwaachilia huru vijana sita waliokuwa wametekwa nyara.

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah

‘Ukaribu wao na serikali, na namna walivyokashifu na kulipuuza jambo hilo zito inaashiria kwamba wana taarifa muhimu ambazo zitasaidia mahakama hii katika uchunguzi wa kubaini watekaji ni akina nani,’ chama kinasema katika ombi kilichowasilisha kortini.

Mnamo Desemba 31 Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye alimtaka Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja kufika mbele yake Jumatano Januari 8, kuhusu vijana hao waliotoweka.

Watano kati ya vijana hao Billy Mwangi, Peter Muteti, Bernard Kavuli, Gideon Kibet na Rony Kiplang’at, waliachiliwa Jumatatu na kuungana na familia zao.

Kando na Bw Atwoli- katibu mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu), Bw Ichung’wah na Bw Kingi, chama hicho kinataka wabunge watano waitwe mahakamani.

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi. PICHA| MAKTABA

Nao ni Bw Junet Mohammed (Suna Mashariki), Bw Oscar Sudi (Kapseret), Bw Mwengi Mutuse (Kibwezi Magharibi), Bw Didimas Barasa (Kimilili) na Bw Erick Wamumbi (Mathira).

Kinasema wanasiasa hao wametoa matamshi hadharani ambayo kwa kawaida kwa ‘mtu mwenye akili timamu yanaashiria kwamba wanaweza kufahamu watekaji nyara ni nani’, au wanaweza kushiriki katika vitendo haramu vya kuwateka nyara Wakenya wasio na hatia.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*