Raila ashinde au abwagwe AU ataathiri pakubwa siasa Kenya – Taifa Leo


JUMAMOSI Februari 15, 2025, labda ndiyo siku muhimu zaidi katika maisha ya kisiasa yaliyosalia ya Bw Raila Odinga.

Ndiyo siku ambapo marafiki na maadui zake wanatarajiwa kufurahia au kutamauka mno.

Kisa na maana? Uchaguzi uliotarajiwa sana wa uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) utafanyika  jijini Addis Ababa, Ethiopia, na Bw Odinga ni mmoja wa wawaniaji watatu.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimeenea mtandaoni tangu mwaka jana kuhusu siku hii, hakuna uchaguzi wa AUC ambao umewahi kuibua msisimko mkubwa kama wa leo.

Kwa sababu gani? Bw Odinga ni mwaniaji, na hakujawahi kuwa na mwaniaji mwingine mashuhuri kama yeye. Mnyonge mnyongee na haki yake umpe; Bw Odinga anapotia nia kuwania wadhifa wowote, hata nje ya Kenya, tarajia msisimko.

Ni mtu mwenye hulka ya ajabu ya kufufua taasisi kutokana na kuwepo kwake tu. Si ajabu Orange Democratic Movement (ODM) kimesalia kuwa chama kikuu cha kisiasa nchini Kenya. Afrika inamjua, kwa heri na kwa shari. Inategemea unamsema na nani.

Unaposoma makala hii, serikali ya Kenya – ikiongozwa na Rais William Ruto – iko jijini Addis Ababa ikilenga kumsaidia Bw Odinga kutwaa wadhifa huo wa AUC.

Uwepo wa Dkt Ruto huko, hasa akimpigia debe Bw Odinga, ambaye alishindana naye katika Uchaguzi Mkuu wa 2022, ni hali ya kuajabiwa si tu nchini Kenya bali pia duniani kote.

Bila shaka naelewa kuna Wakenya wengi ambao wanaomba Bw Odinga ashindwe ili arejee nchini kumsumbua Dkt Ruto katika nyanja za haki za binadamu, demokrasia na kadhalika.

Huo, nakuapia Jalali, ni unafiki wa ibilisi! Si kwamba wanaoshikilia msimamo huo wanaipenda Kenya sana, ndio watake Dkt Ruto afikichwe ili aongoze nchi ipasavyo. Hawampendi Bw Odinga, ndiposa wanataka abwagwe na kubwagika sawasawa.

Wangekuwa wanampenda, basi wangempa urais kitambo sana ili ashughulikie mambo hayo muhimu wanayodhani yanahitaji uwepo wake nchini. Wanataka kumtumia kama kiko ambacho daima hupakua chakula na wala hakili.

Pia hawampendi Dkt Ruto, ila hawana uwezo wa kumsumbua kiasi cha kumtimua Ikulu wala kumkosesha usingizi, ndiposa wanataka kumtumia mtu wasiyempenda, Odinga, kufanya kazi ambayo imewashinda.

Binafsi, sijawahi kumpa Bw Odinga kura yangu kwa kuwa hajanisadikisha kwamba ameiva kisiasa, na sidhani atawahi kuiva, ila nina akili za kutosha kujua kwamba hisia na matamanio yangu hayana ushawishi wowote katika uchaguzi wa leo.

Hata hivyo, naipenda nchi yangu. Siku zote binafsi huona fahari pale Mkenya anaposhikilia wadhifa wowote nje ya nchi. Ziada ni kwamba sijafikisha wivu, chuki na unyimi kiasi cha kumtakia mabaya mtu ambaye anaelekea kustaafu siasa za Kenya.

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*